Okwi
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba Mganda Emmanuel Okwi
anatarajia kwasili nchini kesho kutoka kwao Uganda.
Okwi alikuwa
huko kwa ajili ya kuitumikia timu ya Taifa ya huko ‘The Cranes’ ambayo leo ilikuwa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Zambia.
Ofisa habari
wa Simba Ezekiel Kamwaga amesema kwamba wamekubaliana kimaandishi na nyota
huyo kwamba atatua leo na kuungana na wenzake wanaojiandaa na ligi kuu bara
itakayoanza kutimua vumbi Septemba 15 mwaka huu.
Alisema Okwi
pia anatarajiwa kuwepo kwenye kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani
keshokutwa kuikabili Azam Fc katika mchezo wa kuwania ngao ya Jamii
itakayopigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Kamwaga aliongeza kuwa, kikosi cha timu hiyo
kipo katika hali nzuri kikiendelea na
maandalizi yake kwa kufanya mazoezi katika viwanja vya TCC Chang’ombe
chini ya kocha wake Mserbia Milovan Cirkovic.
Aidha,
Kamwaga aliongeza kwamba mshambuliaji wao mwingine wa kimataifa Mzambia Felix
Sunzu ambaye alikwenda kwao baada ya kufiwa na dada yake naye alitarajiwa
kurejea nchini leo.