KIKOSI cha
timu ya soka ya Yanga kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam jumatano ijayo
kwenda mjini Mbeya tayari kwa mechi yao ya fungua dimba ya ligi kuu bara dhidi
ya Tanzania Prisons ya huko utakaopigwa katika dimba la Sokoine.
Katibu Mkuu
wa Yanga, Mwesiga Selestine amesema kwamba kikosi cha timu hiyo kipo
tayari kwa ajili ya ligi hiyo kwani kupitia mazoezi na michezo ya kujipima
nguvu kimeweza kuimarika.
Alisema
wachezaji wa timu hiyo ambao wanaendelea na mazoezi yao katika uwanja wa shule
ya Sekondari Loyola wapo katika hali nzuri, hali inayowapa matumaini ya kuianza
vema ligi hiyo Septemba 15.
“Kikosi
chetu kipo vizuri na tayari kwa ligi kuu bara…nadhani jumatano timu itaondoka
kwenda Mbeya tayari kwa kuanza ligi kuu”,alisema Mwesiga.
Katika
maandalizi yake ya ligi hiyo, Yanga leo ilicheza mechi ya kujipima ubavu na Moro
United katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Mabatini, Kijitonyama jijini Dar
es Salaam na kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 ambapo mabao mawili kati ya hayo
yalipachikwa na Didier Kavumbagu, huku Shamte Ally na Juma Abdul kila mmoja
akifunga bao moja.
Yanga
inayonolewa na Mbelgiji Tom Saintfiet pamoja na kucheza mechi kadhaa za
kujipima ubavu katika kujiandaa na ligi hiyo ikiwemo ule na African Lyon
iliposhinda mabao 4-0, pia iliiifunga
Coastal Union ya Tanga mabao 2-0.
Aidha, Yanga
ilifanya ziara ya kimichezo nchini Rwanda na kucheza mechi mbili ambapo ilianza
kwa kuifunga Rayon mabao 2-0 kabla ya kuibamiza Polisi ya huko mabao 2-1.