Boniface Wambura, Ofisa habari wa TFF
Tiketi kwa ajili ya mechi ya
Yanga na Simba itakayochezwa keshokutwa (Oktoba 3 mwaka huu) zitaanza kuuzwa
kesho (Oktoba 2 mwaka huu) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam .
Mechi hiyo namba 80 ya Ligi
Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara itachezwa kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam
kuanzia saa 1 kamili usiku.
Vituo vitakavyotumia kuuza
tiketi hizo kuanzia saa 4 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja
wa Taifa, Kituo cha Mafuta OilCom Ubungo, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa
Ohio/Samora, Dar Live Mbagala na Kituo cha Mafuta Buguruni.
Kiingilio cha chini kwenye
mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648 kwenye
uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000. Watazamaji watakaoketi
kwenye viti vya rangi ya bluu ambavyo ni 17,045 watalipa sh. 7,000 kwa tiketi
moja.
Sh. 10,000 ni kwa viti vya
rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 wakati VIP C inayochukua watazamaji 4,060
itakuwa sh. 15,000. Kwa upande wa VIP B tiketi ni sh. 20,000 na VIP A yenye
watazamaji 748 tu kiingilio kitakuwa sh. 30,000.
Wakati huo huo, mwamuzi
Mathew Akrama kutoka Mwanza ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Waamuzi wasaidizi
ni Samuel Mpenzu kutoka Arusha na Ephrony Ndissa wa Dar es
Salaam wakati mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam .
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)