MCHEZO WA MASUMBWI, TAA INAYOZIZIMA – SEHEMU YA TANO



Na Onesmo Ngowi


Masumbwi au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea………………………………….!


 Kama nilivyokwisha kusema, kuna mashirikisho mengi ya ngumi dunia kwa sasa. Baadhi ya mashirkisho haya ni:  Baraza la Ngumi Duniani (WBC), Chama Cha Ngumi Duniani (WBA), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF), Umoja wa Ngumi Duniani (WBU), Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF),

Mengine ni Umoja wa Ngumi wa Kimataifa (IBU), Baraza la Ngumi la Kimataifa (IBC), Chama cha Ngumi cha Kimataifa (IBA), Jumuiya ya Ngumi ya Kimataifa (IBO) Jumuiya ya Ngumi ya Dunia (WBO), Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madoal (CBC), Chama cha Ngumi cha Kitaifa (NBA). Shirikisho la Kimataifa la Ngumi za  Ridhaa (IABA), Shirikisho la Wanawake la Ngumi la Kimataifa (WIBF) na mengine mengi....!

Mashirikisho haya yana matawi katika mabara mbalimbali. Kila shirikisho lililotajwa hapo juu lina taratibu, kanuni na sheria za kuuendesha mchezo wa ngumi. Japokuwa sheria hizi kama nilivyokwisha sema zinafanana.


Katika kuucheza mchezo wa ngumi wachezaji wawili wanapanda kwenye ulingo uliozungushiwa kamba tatu au nne. Mara nyingi vipimo vya ulingo vinatofautiana kati ya ngumi za ridhaa na kulipwa. Lakini pamoja na tofauti hizo vipimo vya ulingo huanzia futi 12 hadi 20 nikiwa na maana ya 12 kwa 12 za mraba na kuendelea mpaka 20 kwa 20.

Ulingo mwingi wa ngumi za ridhaa ni futi 17 kwa 17 ambapo wa ngumi za kulipwa huwa ni 18 kwa 18. Lakini ulingo unaotumika kwa mapambano ya ngumi za uzito wa juu huwa kati ya futi 18 kwa 18 au 20 kwa 20!

Mchezo wa ngumi huwakutanisha mabondia wawili waliovaa glovu mikono yote miwili zenye uzito sawa kufuatana na uzito wao. Mabondia hawa  hurushiana masumbwi kwenye sehemu zilizokubalika. Sehemu hizi zinaanzia juu ya mkanda kiunoni hadi utosini. Bondia haruhusiwi kumpiga mwingine kwenye kisogo.

Mabondia wote wanatakiwa warushe ngumi zilizokunjwa vizuri na zinazopiga eneo lililolengwa barabara. Kuna majaji watatu ambao wanatakiwa wakae kwenye pembe tatu chini ya ulingo.

Hawa ndio watakuwa wanatoa pointi kwa kila bondia kufuatana na uchezaji wake. Kwenye ngumi za ridhaa pointi  huwa zinatolewa wa kompyuta baada ya jaji mhusika kubonyeza kidude fulani kila bondia anapompiga mwenzie.

Katika ngumi za kulipwa majaji wanatakiwa waangalie jinsi mabondia wanapocheza na kutoa pointi kufuatana na wanavyocheza. Baada ya kila raundi bondia aliyeshinda hupewa pointi 10 dhidi ya 9 za aliyeshindwa.

Kama bondia mmoja aliangushwa au kuhesabiwa wakati akicheza kwa sababu ya kupigwa sana, pointi zake zinaweza kuwa 10 kwa aliyeshinda na 8 au 7 kwa aliyeshindwa raundi.

Kila baada ya raundi raferii hupita kwa kila jaji na kuchukua vifaratasi wanavyotumia kutoa pointi na kumpelekea kamisaa wa pambano ambaye kwa kawaida hujumlisha pointi za kila raundi na kutangaza mshindi. Refarii ndiye anayeweza kuamuru bondia akatwe pointi anapoona kuwa amacheza rafu!

Mbali na refarii na majaji kuna Kamisaa anayesimamia pambano na kujumlisha pointi zote toka kila jaji ili kumpata mshindi. Kamisaa ndiye kwa kawaida hutoa mshindi atakayetangazwa.

Mpiga kengele ambaye hutakiwa apige kengele kila raundi inapoanza na inapomalizika. Mtunza muda (Timekeeper) anayeangalia muda unaotumika kucheza na kupumzika kila raundi ya pambano.

Watu wengine muhimu kwenye mpambano ni makocha na masekonda wa kila bondia. Watu hawa husimama kwenye kona ya kila bondia kumpa huduma muhimu kama maji, kumfukuzia hewa, kumfuta jasho na kumpa ushauri wa  alivyocheza raundi iliyoisha na mawaidha ya jinsi atakavyocheza kila baada ya raundi.

Kuna pia madaktari ambao hutoa huduma kwa bondia wakati wa mpambano. Daktari pia ana uwezo wa kumshauri refarii amalize mpambano anapoona kwamba mmoja wa mabondia anaumia vibaya na maisha yake yapo hatarini.

Cutman ni mtu anayemhudumia bondia kwenye sehemu zilizokatika kichwani. Mara nyingi cutman ni watu walio na uwezo wa kuziponyeza mikatiko isitoe damu na kumdhuru bondia asiweze kuendelea na mpambano.

Katika nchi zilizoendelea kama nchi za Ulaya, Amerika, Asia na hata Afrika ya kusini karibu kila bondia ana Cutman wake. Hii inatokana na umuhimu wa kumjua bondia vizuri na umbile la uso wake hivyo kuifanya kazi ya cutman kuwa raisi kidogo. Cutman anajua fika jinsi ya kuziziba (kuzuia damu isitoke) majeraha ya usoni ya bondia wake. Iaendelea………………………….!

Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail:ibfafrica@yahoo.com  

Post a Comment

Previous Post Next Post