Ezekiel Kamwaga, ofisa habari wa Simba
WAKATI mechi ya mahasimu wa soka nchini Simba na Yanga
ikirindima kesho , klabu Simba imetoa angalizo kwa mwamuzi wa mchezo huo Mathew
Akrama wa Mwanza kufuata sheria 17 za mchezo.
Timu hizo zitakutana kwenye uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kuanzia saa
moja kamili usiku.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema wameshangazwa na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF),kumpanga Akrama kuchezesha mechi mbili mfululizo za
Yanga katika hiyo.
Alisema katika mchezo huo wa Jumapili
ambao Yanga ilicheza na African Lyon, awali Tff ilikuwa imepangwa mwamuzi Amon
Paul wa Mara, kabla ya kumbadilisha na kumuweka Akrama.
“Kwa hali kama hiyo lazima tupate na
wasiwasi kidogo, ila yote kwa yote tunamuomba mwamuzi afuate sheria 17 za
mchezo kwani mechi hiyo inagharimu
maisha ya watu wengi sana sasa asije akachafua hali ya hewa,”alisema.
“Kuna hupoteza fahamu,maisha, kuweka rehani nyumba zao, mali zao kucheza kamari, na
wanaliwa au kuna viongozi wengine wamewahi kutimuliwa madarakani kwa sababu ya
kufungwa na Simba na Yanga.
Kwa hiyo, hii mechi ina mambo mengi
sana, sasa sisi tunamuomba Akrama asiue watu, asifanye watu wakaliwa, asifanye
watu wakapata mateso yasiyo na sababu,”alisema.
“Pia mwamuzi akumbuke mechi inarushwa
‘live’ na SuperSport hivyo ambayo inaonekana duniani kote, hivyo kama akifanya
vizuri itamsaidia kukuza taaluma yake na kupata ofa ya kuchezesha katika mechi
ama mashindano makubwa,”aliongeza Kamwaga.
Katika mchezo huo Akrama atasaidiwa na Samuel Mpenzu kutoka Arusha na Ephrony Ndissa
wa Dar es Salaam wakati mwamuzi wa mezani ni Oden Mbaga pia wa Dar es Salaam.
Kuhusiana na maandalizi ya mchezo huo,
Kamwaga alisema kikosi chao kipo katika hali nzuri na cha kutia matumaini ni
kwa mshambuliaji wao Haruna Moshi ‘Boban’ aliyekuwa akiugua Malaria kuanza
mazoezi juzi hivyo kocha ndiye atakayeamua kama atampanga ama la.
Kamwaga aliongeza kuwa wamejipanga kuendeleza
ubabe kwa mahasimu wao hao kwa kuwafunga mabao mengi zaidi ya yale 5-0
waliyowafunga katika msimu uliopita wa ligi hiyo na kusema kuwa pamoja na
kuwakosa nyota wao, Emmanuel Okwi na Amir Maftah katika mchezo huo hilo si
tatizo.
“Tuna silaha za maangamizi za kutosha
ambazo kocha atazishusha katika mchezo
huo, hivyo tunatuma salamu kwa Yanga kwamba wasubiri zawadi nyingine ya
mabao”,Alisema