Na Dina Ismail
MSIMU wa 2012/2013 wa Ligi Kuu Soka
Tanzania Bara ulikuwa mbaya kwa Simba ambayo ilikabiliwa na mithani ya hapa na
pale, lakini kubwa lilikuwa ni kupokwa ubingwa wa ligi hiyo na mahasimu wao,
Yanga.
Dalili za kupoteza ubingwa huo zilianza kuonekana tangu mzunguko wa
kwanza baada ya timu kutokuwa na matokeo ya kuridhisha huku kocha mkuu wa
wakati huo, Milovan Cirkovic, akiahidi neema baadaye lakini hali haikuwa hivyo.
Ndipo uongozi ukaamua
kumfuta kazi Milovan na kumuajiri kocha Mfaransa Patrick Liewig ambaye
aliichukua timu katika mzunguko wa pili wa Ligi hiyo, lakini matokeo yake naye
hakuweza kufua dafu na mwisho wa siku, Simba ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya
tatu.
Baada ya kumalizika kwa
ligi hiyo uongozi wa Simba chini ya Mwenyekiti wake Alhaj Ismail Aden Rage
ulijaribu kuangalia mustakabali mzima wa benchi la ufundi la timu hiyo na ndipo
ulipoamua kumpa jukumu hilo kocha mzawa, Abdallah ‘King’ Kibaden.
Kibaden ambaye alikuwa
akiinoa klabu ya Kagera Sugar si mara yake ya kwanza kuifundisha klabu ya
Simba, kwani amekuwa akifanya hivyo kwa nyakati tofauti.
Ikumbukukwe kuwa Simba
imepata katika makocha tofauti wazawa wakiwemo Athuman Juma Kalomba, Mohammed
Kajole, marehemu Syllersaid Mziray na wengineo.
Lakini kwa zaidi ya miaka
10, ni Mziray ndiye aliyeweza kuipatia mafanikio.
Simba ilipitia kipindi
kigumu katika tangu mwaka 1997 kabla
ya mwaka 2001.
Ilipopata tiketi ya
kushiriki michuano ya Kombe la Washindi na hilo liliwezeshwa chini ya Mziray.
Hivyo, Kibaden ambaye pia
kwenye mlolongo wa makocha wazawa waliopata kuitumikia Simba yumo katika
orodha, kwa sasa ana deni kwa mashabiki wa Simba la kuhakikisha anarudisha
historia ya marehemu Mziray.
Hilo linawezekana kwani kwa
uwezo na uzoefu wa Kibaden, kama atapewa ushirikiano atarejesha matumaini ya
mashabiki wa Simba kwa timu yaliyoanza kupotea tangu mwaka 2011 kwa timu
kufanya vibaya katika mechi zake.
Kwamba, Kibaden ana uzoefu
mkubwa na ufundishaji na hasa ikizingatiwa kuwa katika timu alizopata
kuziongoza, kiwango cha wachezaji kilikuwa cha kuridhisha sana na hatimaye kuony
esha ushindani mkubwa
katika michezo yake.
Simba imempa jukumu hilo Kibaden baada ya kuwa na imani naye kubwa sana , ambapo anaifanya
kazi hiyo akisaidiwa na mzawa mwenzake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Tangu ajiunge na Simba
mwezi Mei mwaka huu, Kibaden amekuwa katika mkakati mkubwa wa kuhakikisha
anaipatia mafanikio timu hiyo ndani na nje ya nchi.
Aidha kwa kuonyesha kuwa
wazawa wanaweza, Kibaden ameonyesha kutaka kutoa nafasi zaidi kwa wachezaji wa
Tanzania akiamini kwamba wana vipaji na uwezo mzuri isipokuwa hawapewi nafasi
uwanjani.
Kama hiyo haitoshi,
Kibaden amesema anahitaji zaidi wachezaji wanaojituma uwanjani sambamba na kuwa
na nidhamu ambayo ni jambo la muhimu kwa wachezaji katika mafanikio yao ya
uwanjani.
Kwa sasa Simba iliyoanza
kuonyesha uhai, imekuwa katika maandalizi yake ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania
Bara unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti hivyo ndio hapo mashabiki
watakapoanza kutaka kuona mafanikio ya kocha huyo.
HISTORIA
Kibadeni alizaliwa Oktoba
11, 1949 jijini Dar es Salaam ambapo akianzia kucheza soka tangu akiwa mdogo.
Mwaka 1969, alijiunga na
Simba (wakati huo Sunderland) akitokea Kahe Republic ya Mtaa wa Kongo na
Mchikichi, Kariakoo.
Mwaka 1974 alilifunga bao
la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Hearts Of Oak ya Ghana nchini Ghana
katika Robo Fainali ya Kwanza ya Klabu Bingwa Afrika, kabla ya kuing’oza Simba
kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika hadi sasa.
Mwaka 1975 aliiongoza
Simba kuwa ya kwanza kubeba Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
michuano ambayo ilichezwa jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1977, Kibadeni, aliifungia
Simba mabao matatu peke yake katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Yanga SC.
Mwaka 1978 aliondoka
Simba na kwenda kuwa kocha mchezaji wa Majimaji ya Songea na kuing’arisha
vilivyo.
Mwaka 1993, aliiwezesha
Simba kufika Fainali ya Kombe la CAF akiwa kocha, rekodi ambayo haijavunjwa
hadi leo ikiwa ni miaka 20 baadaye.
Kibaden ni muumini mzuri
wa dini ya Kiisalmu ambapo mwaka 2011 alikwenda Hijja.
Safari hii ametua Simba
akitokea Kagera Sugar alikoipatia nafasi ya nne katika Ligi Kuu, akiwa na
mkakati wake maalumu katika usajili kwa nyota wa kigeni.
Kibadeni aliyeibuka Kocha
Bora wa Ligi Kuu katika msimu huu, amekuwa akisajili mchezaji kwa uwezo wake
dimbani si umaarufu wa jina au kwa vile anatoka nje.
Hata hivyo, Kibadeni
anakabiliwa na mtihani mgumu wa kudhihirisha ubora na nafasi ya makocha wazawa
katika soka la Tanzania kwani ametua Simba akichukua nafasi ya Milovan Cirkovic
raia wa Serbia.
Hiyo ni kutokana na
ukweli kuwa kwa vile Simba ni miongoni mwa klabu tatu bora nchini, huku akiwa
mzalendo pekee katika kapu hilo, ni nafasi yake kuonesha uwezo dhidi ya Ernie
Brandts (Yanga) na John Stewart Hall (Azam).
Ni wazi Kibadeni ana
nafasi ya kudhihirisha uwezo wa makocha wazawa katika soka ya Tanzania kutokana
na ukweli kuwa ni muda mrefu Yanga na Simba zimekuwa chini ya makocha wa kigeni.
Ndivyo ilivyo pia kwa
Azam ambayo tangu ianze kucheza Ligi Kuu, haijawahi kunolewa na mzalengo kama
kocha mkuu wake, isipokuwa kutoka Uingereza na Ureno.
Namaliza kwa kusema sina
hofu na uwezo wa Kibadeni katika ufundishaji kwani mbali ya uwezo na uzoefu, ni
kocha anayewajua vizuri wachezaji wa Tanzania na Ligi Kuu kwa ujumla. Kila la
kheri.