Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara
msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua vumbi Agosti 24 mwaka huu kwa timu zote 14
kuwa viwanjani katika miji saba tofauti.
Hata hivyo, kabla ya ligi hiyo kuanza kutakuwa na mechi ya
kufungua msimu (Ngao ya Jamii- Community Shield) kati ya bingwa mtetezi Yanga
na Makamu bingwa Azam itakayochezwa Agosti 17 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam .
Mechi za VPL za Agosti 14 mwaka huu zitakuwa kati ya Yanga
na Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mtibwa Sugar na Azam
(Uwanja wa Manungu, Morogoro), na JKT Oljoro na Coastal Union
(Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).
Nyingine ni Mgambo Shooting na JKT Ruvu (Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga), Rhino Rangers na Simba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi,
Tabora), Mbeya City na Kagera Sugar (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya),
na Ruvu Shooting na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani).
Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Novemba 3 mwaka
huu wakati wa pili utamalizika Aprili 27 mwakani. (Ratiba ya mzunguko wa kwanza
na wa pili imeambatanishwa- attached).