KLABU ya Al Markhiya Sports Club ya
Doha, Qatar imetuma barua kwa uongozi wa Simba ukiomba umruhusu kiungo wake
Mwinyi Kazimoto kujiunga na timu hiyo baada ya nyota kufanya vizuri katika majaribia
yake hivi karibuni.
Habari za uhakika zinasema, Kazimoto
aliyekwenda Qatar wiki iliyopita kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa
katika klabu hiyo, ameshafanyiwa vipimo vyote hivyo kinachotakiwa ni kibali tu
kwa ajili ya kuichezea timu hiyo iliyoasisiwa mwaka 1995 ambayo sasa inacheza
Ligi Daraja la Pili.
Japo nyota huyo aliondoka bila
idhini ya viongozi wa Simba wala wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kutokana
na kuondoka nchini akitokea kambi ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Al Markhiya imeiangukia Simba kuomba ridhaa
yake.
Tanzania Daima ilipoutafuta uongozi
wa Simba kuhusu jambo hilo, kiongozi mmoja wa Simba alikiri kuwepo kwa barua
hiyo iliyoandikwa na Mohamed Abu Ali, lakini wenye mamlaka juu ya uamuzi huo ni
viongozi wa juu wa klabu.
“Kweli kuna hiyo kitu, lakini
siwezi kulizungumzia kwa undani zaidi kwani sina uamuzi juu ya hili na hasa
ikizingatiwa mazingira ambayo mchezaji mwenyewe aliondoka sasa tuwaachie
viongozi wenye mamlaka,”alisema
Hata hivyo hakuna kiongozi yoyote
wa juu wa Simba aliyeweza kupatika jana baada
ya kutopokea simu zao za viganjani.
Kama Kazimoto atapata baraka kutoka
kwa uongozi wa Simba atakuwa ni miongoni mwa nyota wa Tanzania wanaopata ulaji
wa kutakata kupitia soka la kulipwa.