WADAU WA SOKA SONGEA KUJADILI UREJESHWAJI WA MAJIMAJI LIGI KUU TANZANIA BARA


Kampuni ya Tanzania Mwandi ikishirikiana na Majimaji FC, imeandaa mkutano wa wadau wote wa soka mkoani Ruvuma chini ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mh. Said Mwambungu, mkutano utakaofanyika katika ukumbi wa Centenary tarehe 10. 08. 2013, kuanzia saa 2 asubuhi.
Lengo kubwa la mkutano ni kurejesha makali ya 1985, 1986 na 1998 kwa klabu ya soka ya Majimaji kwa kuiunda upya kiuchumi chini ya mfumo wa Kampuni, kuijengea uwezo wa kimkakati na kiuendeshaji ili iweze kushiriki kwa mafanikio Ligi Daraja la Kwanza na hatimaye kurejea Ligi Kuu msimu ujao.
Itakumbukwa kuwa Majimaji FC ni klabu ambayo imezalisha magwiji wengi wa soka Tanzania kama Abdala Kibadeni ‘Mputa’, Madaraka Suleimani ‘Mzee wa Kiminyio’, Peter Tino, Steven Mapunda ‘Garincha’, Hamis Gaga, Idd Pazi, Omary Hussein ‘Machinga’ na Mdachi Kombo na ni klabu ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa kwa Simba na Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya Habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Mwandi, Bwana Teonas Aswile amewaalika wafadhili na wadau wote wenye mapenzi mema na Majimaji FC kujitokeza na kushiriki katika zoezi la mjadala wa muundo mpya wa Majimaji na hata kununua hisa kwani sasa Majimaji Kampuni haitakuwa na longolongo zozote. 
“Binafsi nawahimiza wafadhili wa soka kwamba hii ni fursa adimu nyingine ya kuwekeza fedha zao mahali salama. Majimaji itakuwa ikiendeshwa kikampuni na miradi mbalimbali itaanzishwa na klabu ikiwemo upande wa ukandarasi na kuuza wachezaji nje ya nchi. Kwahiyo atakayenunua hisa atafaidika mara mbili.” alisema Teonas Aswile.
Akizungumzia wachokoza mada wakuu wa Majimaji Revival Conference, Aswile amesema kuwa Wakala wa Kimataifa wa FIFA na Mwanasheria Maarufu nchini, Dkt Damas Ndumbaro pamoja na Bwana Silas Mwakibinga, mhasibu na mdau mkubwa wa michezo ambaye ameshashika nafasi mbalimbali.
Kwa sasa maandalizi kwaajili ya Mkutano wa Wadau wa Majimaji FC “Wanalizombe” yanaendelea vyema na wanaohitaji taarifa wanaweza kuwasiliana na Bwana Nasib Mahinya kwa 0655 468800.

Pia viongozi wa Majimaji FC kama Katibu Mkuu Majimaji FC 0752 622887

Post a Comment

Previous Post Next Post