.Baada ya kukonga nyoyo za mashabiki katika robo fainali iliyoshuhudia makundi manne yakitolewa katika mashindano yanayoshirikisha makundi mbalimbali ya kucheza ya Vodacom Dance 100%, moto mwingine unatarajiwa kuwashwa jumapili hii ya mwisho wa wiki katika viwanja vya Don Bosco vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Nusu fainali hizo zitashuhudia makundi 11 yakichuana vikali ambapo makundi matano yatatinga kwenye ngazi ya fainali.Akizungumzia kuhusu nusu fainali hiyo, Msimamizi wa mashindano hayo, Happy Shame alisema kuwa kazi ya mchujo huo itakuwa siyo rahisi kabisa na ni ngumu kwa majaji kutokana na ushindani mkubwa uliopo kati ya makundi yaliyobaki.
“Ushindani katika makundi haya yaliyobaki ni mkubwa sana ukizingatia makundi haya tayari yameshapata mafunzo kutoka BASATA na wadau wengine wa mchezo wa kucheza (dance), Ugumu wa kazi kwa majaji ulionekana hata wakati wa robo fainali ambapo walilazimika kupitisha makundi 11 badala ya makundi 10 ambayo ndio yaliyotakiwa kupitishwa awali,” alisema Shame.
Shame aliongeza kuwa makundi matano yatakayochaguliwa mwishoni mwa wiki hii na kutinga ngazi ya fainali ambapo tarehe ya fainali hizo itatangazwa na hatimaye kumpata mshindi atakayeibuka na kitita cha shilingi milioni 5 toka kwa wadhamini wakuu wa mashinano hayo Vodacom Tanzania.
Kwa upande wa udhamini, Kelvin Twissa, Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom nchini, alisema kuwa kampuni yake inafurahia kuwa sehemu ya utoji wa ajira na huduma bora kabisa kwa wateja wake na anatoa wito kwa wateja wa kampuni hiyo kutumia huduma ya Cheka Bombastic wakati wowote wa burudani wanaopatiwa na vijana hao pale Don Bosco na aliahidi kuendelea kuunga mkono mashindano hayo.
“Vodacom tunaendelea kuvumbua vipaji kwa vijana wa kitanzania, kwa kuendelea kuunga mkono michezo na shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana wa kitanzania, Mashindano ya kucheza ni mapya kabisa hapa nchini kwetu na ni fursa nyingine nzuri kwa vijana wa kitanzania hivyo basi tunaona fahari kuwa sehemu ya mashindano haya.”
Makundi yatakayochuana katika ngazi hiyo ya nusu fainali ni; Wakali sisi, Get dancers, The winners, Best friends, The WT, The chocolate, DDI Crew, Ikulu vegas ,Makabe, Takeover, Pambana Squad.