NYOTA YA JAHA YAMUANGUKIA KAPOMBE

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wana habari.
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, anapenda kuwatangazia wana Simba na wapenzi wa soka kwa ujumla kwamba klabu imefanikiwa kumuunganisha mchezaji wake, Shomari Salum Kapombe, na klabu ya soka ya AS Cannes ya Ufaransa.
Katika mkataba huo mpya na wa aina yake kuwahi kufanywa na klabu yoyote ya Tanzania, Simba imekubali mchezaji huyo achezee timu hiyo iliyo katika ligi daraja la nne la Ufaransa kwa makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza ndani ya miaka miwili kutoka sasa.
Timu hiyo itamgharimia Kapombe kwa kila kitu wakati atakapokuwa nchini Ufaransa. Endapo Kapombe atauzwa kwenda katika timu nyingine yoyote, Simba itapata gawio lake kupitia mauzo hayo na lengo la mchezaji huyo kubaki Ufaransa ni pia kumtengeneza awe bora zaidi kuliko alivyo sasa.
“Kwenye makubaliano hayo, Simba haitapata chochote kwa sasa. Isipokuwa endapo Kapombe atapata timu, Simba itapata mgawo wake kutoka katika mauzo hayo. Makocha wa Ulaya wamebaini kwamba Shomari ni mchezaji mzuri sana lakini anahitaji kuboreshewa vitu vichache kabla hajawa mchezaji mkubwa wa kutumainiwa na vilabu vikubwa,” alisema Rage.
Rage alisema katika mkataba huo mpya wa Kapombe, Simba imeangalia zaidi maslahi ya taifa na ya mchezaji kuliko ya klabu kwa vile kama mchezaji huyo atapata nafasi Ulaya, hilo litafungua milango kwa wachezaji wengi wa Kitanzania ambao kwa sasa hawapati fursa Ulaya.
Wakala wa Kapombe, Denis Kadito, alisema ingawa Kapombe ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa jina la Tanzania kumekuwa kikwazo kikubwa kwa kupata kwake nafasi ya moja kwa moja na ndiyo maana imebidi aanzie kwenye hatua ya chini.
“Ofa hii ya Cannes ni nzuri kwa sababu timu hiyo huwa inacheza na timu za akiba za vilabu vyote vinavyoshiriki katika Ligi Kuu ya Ufaransa na hivyo atakuwa anaonwa na mawakala wa timu kubwa kila wiki. Hii itamsaidia kupata timu kubwa mapema ndani ya msimu mmoja kutoka sasa,” alisema Kadito.
AS Cannes ni mojawapo ya vilabu vikubwa nchini Ufaransa na ni maarufu kwa kuibua vipaji vikubwa. Miongoni mwa nyota maarufu wa Ufaransa waliowahi kupita katika klabu hiyo ni Patrick Vieira, Zinedine Zidane na Luis Hernandez.
Klabu hiyo inafahamika kwa kuwa na miundombinu imara ya kumwezesha mwanasoka kijana kukuza uwezo wake na ni matarajio ya Simba Sports Club, Kadito, Cannes na Kapombe mwenyewe kwamba atakuwa mchezaji bora zaidi kuliko sasa katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka sasa.
Kutokana na mkataba huo wa Kapombe na Cannes, Simba sasa imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa muda wa miaka mitatu zaidi, kwa vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili mwakani. Kama Kapombe hatafanikiwa kupata timu katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa, atarejea katika klabu ya Simba kuendelea na majukumu yake.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari

Simba SC

Post a Comment

Previous Post Next Post