WIZARA ya Habari, Utamaduni,
Vijana na Michezo imekiri kwamba mchakato wa marekebisho ya Katiba ya
Shirikisho la soka Tanzania (TFF) yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura Julai
13, una dosari na ndio maana imekwama kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni
siku moja tu tangu Gazeti hili liandike habari ya katiba hiyo kukwama kwa
msajili kutokana na marekebisho kupitishwa pasipo kupigiwa kura kama ibara ya 30 (iii) inavyotaka pamoja.
Dosari nyingine ambayo
ilielezwa awali iliyomfanya Msajili Mercy Rwezaura kusita kupisha marekebisho
hayo, ni kitendo cha TFF kuunfa Kamati za Maadili kabla ya katiba hiyo kupata
baraka rasmi za ofisi yake.
Akizungumza na Tanzania Daima
kwa njia ya simu kutokea Jimboni kwake Mvomero, Morogoro, Naibu Waziri Amos
Makala, alikiri kuarifiwa jambo hilo
na Msajili kuwa mchakato wa upitishaji
marekebisho hayo una dosari kwa mujibu wa katiba.
“Ni kweli nimejulisha na
ofisi ya Msajili kuwa kuna dosari, tena tunataka TFF wenyewe wawaeleze ukweli
Watanzania kwa sababu wakati mwingi
serikali imekjuwa ikitupiwa lawama kwamba inataka kuharibu mambo,” alisema
Makala.
Akifafanua zaidi, Makala
alihoji inawezekana vipi marekebisho ya uundwaji wa Kamati za Maaadili kabla ya
kupata baraka za Ofisi ya Msajili, wao TFF tayari wameshaunda Kamati husika na
kutangaza wajumbe wake.
“Hivi inaingia akilini kweli,
ninyi mmefanya mabadiliko ya katiba ili itambue uwezpo wa Kamati za Maadili na
mmepeleka kwa Msajili ipate baraka, lakini kabla haijapita, ninyi mnaziunda
kamati,” alihoji Makala.
Alipoulizwa juu ya hatma ya
uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo
ambao umetakiwa uwe umefanyika hadi kufikia Oktoba 30 mwaka huu, Waziri Makala
alisema lolote litakalotokea mbelke ya safari, Serikali haipaswi kulaumiwa.
“Kuhusu ukomo wa muda ambao
Fifa (Shirikisho la soka la Kimataifa) limetaka kwa kipindi fulani uchaguzi
mkuu uwe umefanyika, sisi hilo
tunawaachia TFF wenyewe waamue nini cha kufanya, sisi tunaangalia sheria na
taratibu za nchi zinasema nini,” alisema.
Utata huo katika marekebisho ya
Katiba yaliyofanywa kwa maelekezo ya Fifa, ni mwendelezo wa mchakato wa
uchaguzi wa shirikisho hilo
kuwa na dosari kwani
awali ulipangwa kufanyika
Februari 24, lakini ukasimamishwa.
Hata hivyo, wataalamu wa
masuala ya soka, wanasema pamoja na mapungufu hayo, katiba hiyo inaweza kupitishwa na Msajili,
lakini kabla haijatumika kwenye uchaguzi, itapaswa kupata baraka za Mkutano
Mkuu kisha kugongwa mhuri siku hiyo.