KOCHA Mkuu wa Yanga,
Ernie Brandts, anatarajiwa kurejea nchini kesho, kabla ya kukiongoza kikosi
chake kuivaa Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam ,
keshokutwa.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa Mholanzi
Brandts ameishamaliza kozi ya siku ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na kwamba
kwa sasa yu tayari kurejea kukiandaa kikosi kuelekea ufunguzi wa msimu wa Ligi
Kuu Tanzania Bara.
“Kikosi cha Yanga,
Jumapili kinatarajia kushuka ndani ya Uwanja wa Taifa kucheza mchezo wa
kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi ambayo itakuwa ya kwanza kwa Brandts anayerejea
nchini kesho kutoka mafunzoni Ujerumani,” alisema Kizuguto.
Brandts alikuwa nchini
Ujerumani kwa ajili ya masomo mafupi ya kuongeza muda wa leseni yake ya ukocha
ya UEFA, yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 29 hadi 31, yakihusisha
makocha mbalimbali wenye leseni zinazotambuliwa na shirikisho hilo .
Kizuguto alisema kwamba watautumia
mchezo huo kuwatambulisha wachezaji wote wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu
mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom na klabu bingwa barani Afrika.
Nyota wapya waliotua Jangwani
ni pamoja na Deogratius Munishi 'Dida,' Rajab Zahir, Hamis Thabit, Shaban Kondo,
Mrisho Ngassa, Hussein Javu na Reliants Lusajo.
Wakati huo huo, Mweka
Hazina wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kinachoratibu mchezo
huo, Ally Hassan, alisema kuwa taratibu zote zimekamilika.
Hassan alitaja viingilio
kuwa ni sh 15,000 kwa VIP A, sh 10,000 VIP B na C, huku viti vya rangi ya bluu,
kijani na machungwa ni sh 5,000.