UONGOZI wa klabu ya
Simba, umesema haki ya kurusha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kumilikiwa na
Azam TV ni ukombozi wa kiuchumi kwa klabu shiriki na maendeleo ya soka hapa
nchini.
Tamko la Simba, moja ya
klabu kongwe nchini, limekuja siku chache tangu watani wao Yanga, wakatae
udhamini huo kwa hoja mbalimbali, ikiwemo mchakato wa jambo hilo kutowekwa wazi.
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga,
alisema wanaridhia hilo kwa sababu hata kanuni za vyombo vya juu vya mchezo huo,
kama Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Afrika (CAF), na Tanzania (TFF),
ndivyo vyenye haki ya kufanya majadiliano juu ya matangazo ya kwenye
televisheni.
Alisema kwa muda mrefu
klabu zimekuwa zikilalamika kutokuwepo wadhamini, sasa litakuwa jambo la ajabu
timu ipinge udhamini huo kwa sababu ambazo hazina mashiko.
Kamwaga alikwenda mbali na
kuhoji, hao wanaopinga udhamini wa Azam Tv, walikuwa wapi kufanya hivyo wakati
SuperSport ya Afrika Kusini ikionyesha baadhi ya mechi za ligi hiyo bure?
“Tulikuwa na SuperSport
kwa miaka kadhaa wakionesha michezo yote, tena buree…leo hii Azam Tv wanakuja
na sh milioni 100, tunaanza kuleta mizengwe, tunadhani si jambo zuri,” alisema
Kamwaga.
Kamwaga alisema kutokana
na umuhimu wa udhamini huo, klabu zinapaswa kuikumbatia Azam Tv, kwani
utasaidia kuvuta kampuni nyingine kuwekeza kwenye ligi hiyo.
Alisema kama kuna tatizo
la kuzungumza kuhusiana na udhamini huo, wasizungumzie pembeni, hasa
ikizingatiwa kuwa mchakato mzima ulihusisha pia Bodi ya Ligi chini ya
Mwenyekiti wake, Wallace Karia.
Katika hatua nyingine,
Simba inatarajiwa kushuka Uwanja wa Taifa kesho kukwaana na kombaini ya polisi,
ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu itakayoanza
Agosti 24.
Mechi hiyo itakayoanza
saa 10 jioni, viingilio ni sh 20,000 kwa VIP A, 15,000 VIP B, 10,000 VIP C na
5,000 kwa viti vya kijani, chungwa na bluu.