LICHA ya nyimbo alizowatungia baadhi ya wasanii
nyota wa muziki wa bongo fleva kutwaa tuzo, lakini kazi anazozitoa mwenyewe
hazijaweza kumpa umaarufu mkubwa kama kipaji alicho nacho.
Huyo si mwingine, bali ni msanii wa muziki wa
bongo fleva, Hamidu Hafidh Mshinda maarufu kama Ude Ude.
Nyimbo kama ‘Wangu’ ya Lady Jaydee, ‘Maneno
Maneno’ ya Queen Darleen, ‘Bwashee’ ya Baby J, ‘Oyoyo’ Bob Junior na nyinginezo
ni baadhi tu ya nyimbo ambazo zimetungwa na Ude Ude na kutwaa tuzo mbalimbali.
Baada ya kuwawezesha wasanii wenzake kwa tungo
nzuri, kwa sasa Ude Ude ameamua kuweka kando suala la kuwatungia nyimbo wasanii
wengine na sasa kujikita mwenyewe katika uimbaji.
Katika mkakati huo, mwanzoni mwa wiki hii
ameachia ‘singo’ yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘Ngoma Inogile’,
iliyotengenezwa katika studio za Fire Music chini ya mtayarishaji More Fire.
Kama hiyo haitoshi, Ude Ude anatarajia kuizindua
rasmi video ya wimbo huo, Iddi Mosi ndani ya ukumbi wa kimataifa wa Club
Bilicanas uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala hii, Ude
Ude anaeleza kwamba, kwa sasa amejipanga vema kuhakikisha anafika kileleni
katika medani ya muziki wa bongo flava.
“Nimedhamiria vilivyo kuliteka soko la muziki
kwa sasa, tofauti na zamani ambapo nilikuwa natoa nyimbo tu kama kujifurahisha,
nimejipanga vema, hivyo naomba mashabiki mnipokee,” anasema.
Ikumbukwe kuwa kabla ya singo yake hii mpya, Ude
Ude alipata kutoka na nyingine kadhaa, zikiwemo ‘Kujinafasi’ alioutoa mwaka
2009 na ‘Nipe Kidogo’ mwanzoni mwa mwaka huu.
Akifafanua zaidi, Ude Ude anasema tayari ana
nyimbo zaidi ya 60 ambazo amezitayarisha katika studio tofauti, huku
akiwashirikisha wasanii mbalimbali ili kuleta ladha na vionjo tofauti, ambapo
hivi sasa yuko chini ya usimamizi wa Kampuni ya Babuu Kisauji Entertainment.
Akizungumzia safari yake kimuziki, Ude Ude anasema ilianzia mwaka
2002 akiwa na ndugu yake aitwaye Ramadhan Yusuf, ambaye alikuwa akimfundisha
jinsi ya kuandika huku jioni wakifanya mazoezi ya kuimba katika saluni moja
karibu na nyumbani kwao.
Anasema mwaka 2004 alishiriki mashindano ya
muziki yaliyoandaliwa na msanii wa filamu, Dk. Cheni katika ukumbi wa Da West
Park Tabata, akiwa na kundi la Kyudas lililoundwa na wasanii Big Black na Kg
Son na kujikuta wakishinda na kuzawadiwa sh 100,000.
“Baada ya mashindano hayo, nilitulia kabla ya
mwaka 2009 kutoka na singo yangu ya kwanza niliyoipa jina la ‘Kujinafasi’
ambayo iliweza kunitambulisha katika medani ya muziki, ingawa kwa kiasi kidogo
sana,” anasema.
Anasema aliendelea kujikita katika kuwatungia
wasanii wenzake nyimbo kabla ya kukutana na meneja wake wa sasa, Babuu Kisauji,
ambaye alianza kumpa ushauri na ndipo mapema mwaka huu, akaachia singo nyingine
iitwayo, ‘Nipe Kidogo’.
Ude Ude anasema kutokana na kuwa chini ya usimamizi
maalumu, sambamba na kujipanga katika kufanya vema kwenye medani ya bongo
fleva, ameweka pembeni suala la kutungia wasanii wenzake, badala yake atafanya
hivyo kwa mkataba maalumu.
Akiwa na matarajio ya kufika mbali zaidi na
kuwasaidia wasanii wengine, Ude Ude amewataka kupendana na kushirikiana, huku
akiwasisitiza waliopiga hatua kupambana kimataifa badala ya kukaa wakiwadhibiti
chipukizi.
“Waliopiga hatua waangalie mbele kwa kutafuta
soko nje ya mipaka si kukabana na chipukizi, pia tuwe wabunifu, kwani
itatusaidia kusonga mbele na wadau wa muziki watoe sapoti kwa wasanii wote, si
kuangalia huyu anafanya kazi na nani,” anaongeza.
Ude Ude ambaye anavutiwa na msanii Suma Lee,
alizaliwa Machi 3, 1988 jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi Shule ya
Ilala.
Hata hivyo hakuendelea na masomo kutokana na
matatizo ya kifamilia, hasa kukosa mtu wa kumlipia ada kwa ajili ya
kujiendeleza zaidi kielimu.