SIMBA imekataa ofa iliyotolewa na klabu ya Al Markhiya ya Qatar kwa ajili ya kumsajili aliyekuwa kiungo wake, Mwinyi Kazimoto kwa madai kuwa ni ndogo sana ukilinganisha thamani ya mchezaji huyo.
Ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alikiri kwamba
wamepokea ofa kutoka timu ya moja ya Qatar
lakini ni ofa ndogo sana
ambayo hawawezi kuikubali kwani thamani yake haifikii ile waliyomuhamishia
kutoka JKT Ruvu.
Hata hivyo, Kamwaga alisema hawezi kuzungumzia kwa undani
juu ya suala la Kazimoto kutokana na ukweli kwamba bado ana maswali ya kujibu
Watanzania na klabu yake ya Simba kwa ujumla.
“Suala la Kazimoto tumeliweka pembeni kwani tunatarajia
kukaa na TFF kwa ajili ya kumjadili na baada ya hapo mambo mengine kuhusu yeye yatafuata,”alisema
Ikumbukwe kuwa, Kazimoto alitimkia Qatar hivi karibuni baada ya kutoroka katika
kambi ya timu ya Taifa siku ambayo ilikwaanza na Uganda ‘The Cranes’ katika mchezo
wa kuwania kufuzu fainali za Afrika zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi
za ndani (CHAN).
Kazimoto aliyesajiliwa na Simba kutoka JKT Ruvu alikwenda kujaribiwa
na klabu ya Al Markhiya Sc inayoshiriki Ligi daraja la kwanza ya huko na kufuzu
na hivyo wakala wake, Mahmoud Abu Al Ght kuwasiliana na uongozi wa Simba kwa
ajili ya ofa hiyo.