TIMU ya soka
ya Simba inatarajiwa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi SC Villa ya
Uganda mchezo utakaopigwa Agosti 10 katika Uwanja wa taifa jijini Dar es
Salaam.
Mchezo huo
ni maalum kwa klabu ya Simba kuadhimisha miaka 77 tangu kuanzishwa kwake ambapo tayari klabu
hiyo imeanza kufanya kazi mbalimbali za kijamii.
Katibu Mkuu
wa Simba Evodius Mtawala amesema kwamba maandalizi kwa ajili ya mchhezo
huo utakaohitimishwa baada ya tamasha maalum yanakwenda vizuri ambapo Villa watatua nchini keshokutwa.
Alisema
kupitia mchezo huo pia mashabiki wa Simba watapata fursa nyingine ya
kuwashuhudia baadhi ya nyota wake wapya waliosajili na timu hiyo kwa ajili ya
msimu ujao wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara pamoja na michuano mingine.
“Pia katika
tamasha hilo litakaloambatana na burudani mbalimbali, tutatambulisha jezi zetu
mpya tutakazozitumia katika msimu ujao wa ligi,”alisema Mtawala.
Baadhi ya
nyota wapya waliosajiliwa Simba ni pamoja na Mrundi Amisi Tambwe, Waganda
Joseph Owino na Gilbert Kaze na wazawa kama Abdulhalim Homoud, Betram Mombeki
na wengineo.
Simba kwa
sasa ipo kambini kwenye hoteli ya Bamba Beach iliyopo Kigamboni jijini Dar es
Salaam ikiendelea na maandalizi yake chini ya makocha Abdallah Kibaden ‘Mputa’
akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.