Na Dina Ismail
UWEZEKANO wa Uchaguzi Mkuu wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufanyika ndani ya kipindi kilichotakiwa na
Shirikisho la soka Tanzania
(Fifa), ni mdogo, Tanzania Daima imebaini.
Wakati Fifa wakiagiza
uchaguzi huo uwe umefanyika ifikapo Oktoba 30, lakini marekebisho ya katiba
yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa Dharura Julai 13, yamekwama katika
Ofisi ya Msajili wa Vyama na
Klabu za Michezo.
Japo TFF imepanga uchaguzi
huo ufanyika Septemba 29, lakini suala la Katiba hiyo kukwama kwa Msajili,
kunatia shaka kama uchaguzi huo utafanyika kwa
ulitakiwa na Fifa
Wakati kukiwa na ukimya huo, habari
zilizoifikia Tanzania Daima, zinasema kukwama kwa Katiba hiyo katika ofisi ya
Msajili, ni kutokana na dosari mbili kubwa zilizofanywa.
Chanzo chetu kimedokeza kuwa,
dosari ya kwanza ambayo imeifanya ofisi ya Msajili kusita kupitisha marekebisho
hayo, ni staili iliyotumiwa na Mkutano Mkuu kuipitisha Katiba hiyo.
Kwamba, wakati Ibara ya 30
(3) ya Katiba ya Shirikisho hilo ikitaka
marekebisho yapigiwe kura, kuna habari kuwa jambo hilo halikufanywa na wajumbe wa mkutano Mkuu.
Kwa mujibu wa kipengere
hicho, ili marekebisho yawe halali, yapaswa kupata baraka ya zaidi ya asilimia
50 ya idadi ya Wajumbe katika mkutano huo.
“Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya
TFF inatamka wazi ili marekebisho yaweze kuwa halali, yanapaswa kupata baraka
ya asilimia 50 + 1 ya wajumbe walipo ukumbini. Katika uchaguzi ule wa Julai 13,
hili halikufanyika, ilipitishwa kijumla tu,” kilidokeza chanzo chetu.
Habari zinasema, kwa vile
jambo hilo
halikufanyika katika upitishaji wa marekebisho hayo, Ofisi ya Msajili imejikuta
kwenye wakati mgumu kuipitisha hadi kufikia jana, akihoji ilipitishwa kwa
staili ipi kwani utaratibu ni wajumbe kupiga kura.
“Ili marekebisho yaweze kuwa
halali, yanapaswa kuuungwa mkono na asilimia 50+ 1 ya idadi ya wajumbe
waliohudhuria mkutano husika,” kinasomeka kifungu hicho cha tatu cha Ibara ya
30 ya Katiba ya shirikishi hilo .
Habari zinasema, japo Ofisi
ya Msajili ingependa kuona mchakato wa uchaguzi huo unafanyika ndani ya kipindi
kinachotakiwa na Fifa, lakini dosari hiyo imeifanya isite kuipitisha katiba
hiyo haraka kama ilivyokuwa imetarajiwa.
Kinachotishia zaidi uchaguzi huo
kufanyika kwa wakati, ni mchakato mzima kuhitaji muda wa siku zisizopungua 60
kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, hivyo kama
si rasimu hiyo kukwama kwa Msajili, mchakato huo ungepaswa uwe umeanza walau kuanzia
leo.
Aidha, kitendo cha Kamati ya
Utendaji kufanya uteuzi wa Kamati mbalimbali kwa mujibu wa marekebisho yaliyomo
kwenye rasimu inayosubiri baraka za Msajili, ni dosari nyingine ambayo
pia imehojiwa na Ofisi ya
Msajili.
“Ofisi ya Msajili imehoji pia
uundwaji wa Kamati za Maadili umefanywa kwa katiba ipi? Inajiuliza hivi kwa
sababu marekebisho yaliyofanywa bado hayajapata baraka kisheria,” kilisema
chanzo hicho.
Mwandishi wa habari hizi
alipomtafuta Msajili, Mercy Rwezaura kupata kauli yake
juu ya madai hayo, alisema hawezi
kusema lolote kwa vile ofisi yake bado inaendelea kuipitia.
“Kwa sasa siwezi kusema
lolote kwa vile bado tunaendelea kuipitia,” alisema Msajili huyo.
Alipoulizwa juu ya madai
kwamba dosari ndizo zimeifanya ofisi yake ishindwe kupitisha rasimu hiyo kwa
wakati, alisema hana taarifa yoyote na kusisitiza wanaendelea kuipitia rasimu ya katiba hiyo.
Tanzania Daima lilimtafuta
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kujua mustakabali mzima wa katiba na
mchakato wa uchaguzi huo kwa ujumla, alisema bado wanasubiri majibu kutoka kwa
msajili kabla ya mengine kuendelea.
Kuhusu madai ya dosari ya
akidi, Osiah alisema wakati wa kukabibidhi marekebisho hayo kwa Msajili, waliambatanisha
na muhtasari wa mkutano huo ambao unaonesha kila kitu kilichofanywa na wajumbe
wa Mkutano Mkuu.
“Katika katiba tuliyoipeleka
kwa Msajili, tuliambatanisha muhtasari ya wajumbe walioshiriki, sasa sijui
idadi ipi inayohojiwa,” alisema
Kuhusu uteuzi wa Kamati mbili
mpya za Maadili, Osiah alisema kwa mujibu wa katiba hiyo hiyo ya TFF, mabadiliko
yaliyopitishwa huanza kutumika mara moja hata kabla ya kupitishwa na Msajili.
Awali, uchaguzi wa Shirikisho
hilo ulipangwa
kufanyika Februari 24, mwaka huu, lakini ukaota mbawa baada ya Shirikisho la
Soka kutaka iwe hivyo kutokana na
baadhi ya wagombea kulalamika
kuchujwa isivyo halali.
Baada ya Fifa kumtuma mjumbe
wake, Primo Carvaro kuja nchini na kupeleka ripoti, ndipo Shirikisho hilo lilipoagiza uundwaji
wa Kamati mbili za Maadili na kutaka uchaguzi uwe umefanyika hadi ifikapo
Oktoba 30.
Hata hivyo, habari zinasema
pamoja na dosari hizo, Ofisi ya Msajili yaweza
kuipitisha katiba hiyo kwa
sharti la dosari hiyo kifanyiwe kazi katika Mkutano
Mkuu wa Uchaguzi kama ilivyokuwa uchaguzi wa Desemba 27, 2004.