TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Wana habari.
Asalaam Aleikhum.
KATIKA siku za karibuni,
kumekuwapo na mjadala kuhusiana na hatua ya klabu ya Yanga kupinga udhamini wa
Ligi Kuu ya Tanzania unaotarajiwa kufanywa na Azam Media.
Tumeona ni vema tukatoa
msimamo wetu wa pamoja kuhusiana na hatua hiyo ya wenzetu kwa lengo la kuweka
rekodi sawa.
Tunataraji hatua hii ya
vilabu hivi 13 itafunga mjadala huu na tungependa wana habari, kama mtaamua
kuuendeleza, basi muundeleze katika mrengo ambao wadau, yaani sisi vilabu
vinavyoshiriki mashindano hayo, zimeamua kuufuata.
Tunapenda kukumbusha
kwamba kwa muda mrefu, kilio cha vilabu vya Ligi Kuu ya Tanzania vilikuwa ni
ukosefu wa wadhamini na kwa bahati nzuri kuna dalili kwamba Mungu ameanza
kukisikia kilio hicho msimu huu.
Kwa faida ya umma,
tungependa kutoa takwimu za nchi jirani zinazotuzunguka. Kenya, kila klabu
hupata Sh milioni saba za Kenya (sawa na Sh milioni 125 za Kitanzania) kwa
mwaka –fedha ambazo zimeifanya ligi ya Kenya kuwa na uwiano na ushindani wa
kweli (fedha hizo ni mjumuisho wa gharama za matangazo ya televisheni na
udhamini wa bia ya Tusker).
Tanzania leo tunajivunia
kuwazidi Kenya kutokana na udhamini wa Azam ambapo kwa mwaka huu, kila klabu
itapata zaidi ya Sh milioni 170 (Jumla kutoka milioni 100 za Azam na milioni 70
za Vodacom).
Hatuna sababu ya kutaja
viwango vya udhamini kwa nchi nyingine jirani kama Uganda, Burundi, Rwanda,
Zambia nk kwa vile zote zina udhamini wa chini kuliko Kenya.
SuperSport, ambao
wanaliliwa na baadhi yetu, udhamini wao kwa ligi ya Uganda ni dola 350,000
ambazo ni pungufu kulinganisha na dola milioni moja zilizotolewa na Azam Media
hapa nchini.
Ni imani yetu kwamba
udhamini huu utaifanya ligi ya Tanzania kuwa bora kuliko zote za Afrika
Mashariki. Hili litasaidia kutengeneza timu bora ya Taifa ya Tanzania.
Tungependa kutoa
ufafanuzi wa masuala machache ambayo yaliongelewa na wenzetu wa Yanga kama
sababu za kupinga udhamini huu.
BODI YA TPL
Kwa mujibu wa Katiba za FIFA, CAF na TFF, Haki za Televisheni zipo
chini ya FA ya nchi husika. TFF iliamua kukasimu shughuli ya majadiliano kwa
Kamati ya Ligi ambayo ilishirikisha vilabu vyote 14, ikiwamo Yanga na
wawakilishi wake walihudhuria mchakato mzima hadi mwisho.
Hoja ya Yanga kuwa bodi
haina nguvu/Mamlaka kisheria kwa kuwa ni ya mpito inakosa mashiko kwa sababu
kimsingi ni TFF ndiyo iliyoingia mkataba kwa sababu ndiyo iliyopewa mrejesho na
Kamati ya Ligi kwamba mchakato umekwenda sawasawa.
Hoya ya kuwa Bodi ya TPL
iliyoko sasa hivi haina mjumbe hata mmoja aliyeteuliwa kutoka YANGA. Hili si
kweli hata kidogo. Mmoja wa wajumbe wa TPL ni Seif Ahmed almaarufu Seif Magari;
ambaye vyeo vyake ndani ya Yanga vinajulikana.
Kama alikuwa hahudhurii
vikao vya TPL, hilo ni suala la Wanayanga wenyewe kumuhoji kwanini alikuwa
hahudhurii hivyo na hivyo kuinyima klabu yake ushiriki katika mijadala muhimu
kwa maslahi ya soka hapa nchini.
Ifahamike pia kwamba TPL
haikuhodhi mchakato huu bali ilitoa fursa kwa vilabu vyote vya Ligi Kuu
kushiriki ambapo Yanga ilikuwa ikiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wake, Clement
Sanga na Katibu Mkuu, Lawrance Mwalusako.
Hii maana yake ni kwamba
hoja kuwa Yanga haikushirikishwa ni mfu.
Yanga walitumia neno
UTARATIBU WA DUNIA NZIMA wakisema eti hakuna mahala duniani ambapo kampuni
yenye klabu inayocheza ligi husika kupewa mkataba wa udhamini au urushwaji wa
matangazo.
Inaonekana Yanga
hawakufanya utafiti kwani ligi ya Afrika ya kusini ina timu inayoitwa Super
Sports United na inarushwa na kituo cha TV chaSupersports.
Pia majirani zetu Kenya
wana timu inayoitwa Tusker FC huku ligi hiyo ikidhaminiwa na bia ya Tusker.
Tunawashauri Yanga kuwa
ni vema kufanya utafiti kabla ya kuibuka na hoja za namna hii ili kuepuka
kuwapotosha wanachama wao.
Yanga pia katika hoja zao
wamepinga utaratibu wa kugawana mapato sawa. Hoja hii ni ya msingi na
majadiliano yetu yalilitazama hili kwa kina lakini tukaona kwa mazingira ya
Tanzania na uchanga wa ligi yenyewe kwa sasa ni heri kugawana sawa ili pesa kwa
usawa ili itoke kwa wakati na kusaidia vilabu kujiendesha. Yanga wanakosea
wanaposema eti wao wanastahili kupewa zaidi kwa sababu ni klabu kubwa na yenye
mashabiki wengi kwa kuwa sababu hii haitumiki sehemu yoyote duniani.
Tuchukulie mfano wa nchi
ya England ambako ingawa Liverpool ina washabiki wengi kuliko Manchester City
na Chelsea, imezidiwa kwenye mapato ya televisheni na timu hizo.
Hii ni sababu kinachoamu
mapato mwisho wa siku ni kiasi cha mechi za timu ambazo zimeonyeshwa na
televisheni kwenye msimu husika na nafasi ya timu kwenye msimamo wa ligi.
Hata hivyo, ikumbukwe
kwamba nchini England, malipo haya hufanyika baada ya msimu kumalizika na hapo
ndipo watu hukaa chini na kupigiana hesabu za nini kilipatikana. Sasa ukitumia
mfumo huu, ina maada timu zitalazimika kusubiri ligi iishe ili kuangalia
msimamo ya ligi kisha kugawana mapato. Sote tunajua jinsi timu zinavyoteseka
kwa kukosa nauli, posho, mishahara, pesa za kambi nk.
Kwa mazingira yetu ya
Tanzania kwa sasa, mfumo kama huu haufai. Hii ni kwa sababu timu zinahitaji
fedha kuanzia kwenye maandalizi ya mechi ya kwanza na hazikopesheki fedha
kwenye mabenki.
Tanzania inachohitaji kwa
sasa ni ligi yenye ushindani tofauti na sasa ambapo ushindani uko kwa timu
chache zenye uwezo wa kifedha.
Tukizijengea uwezo timu
zote taifa litakuwa na ligi nzuri na hatimaye timu nzuri ya taifa. Pia
itawezesha wadhamini wengi zaidi kuingia kwenye mpira na hivyo timu nyingi
zaidi kufaidika.
Tukifikia huko, tunaweza
kukaa chini na kutazama mfumo wa kugawana mapato utakaokuwa bora zaidi wakati
huo.
Mambo ya Kuzingatia.Tangu
ligi ianze hapa nchini takribani miaka 50 iliyopita, hakuna timu iliyowahi
kulalamikia mfumo wa kugawana mapato sawa kwa kila mechi ambao umekuwa
ukitumika. Mfano mapato ya mlangoni tumekuwa tukigawana sawa na Yanga haijawahi
kulalamika, Pesa za udhamini wa Vodacom tangia ilipokuwa ikidhaminiwa na TBL
hadi leo hii tumekuwa tukigawana sawa na
Yanga haijawahi kulalamika kutaka kupata zaidi kwa kuwa eti ina mashabiki
wengi, pia hata pesa za haki ya matangazo ya Televisheni zilizowahi kutolewa
huko nyuma nailiyokuwa ikiitwa GTV, na Star TV kwa nyakati tofauti pesa
ziligawiwa sawa kwa kila timu.
Hii ni kwa sababu
kikanuni, timu zote zinazoshiriki kwenye ligi ni sawa na zote zinaweza kuwa
bingwa au kushuka daraja.
Ni mdudu gani huyu
aliyeingia kwenye soka ya Tanzania na kuanza kuleta siasa za kubaguana? Baba wa
Taifa alipata kutuasa kwamba dhambi ya ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu.
Ikianza, haitaishia kwenye ligi pekee na itakwenda hadi mahali tusipotaka.
MGOGORO WA MASLAHI.
Yanga imekuwa ikilalamikia uwepo wa kiongozi mwandamizi wa
makampuni ya Bakhresa kwenye bodi ya Ligi na kusema inaleta mgongano wa
maslahi.
Sisi vilabu tunaamini kwamba uwepo wa kiongozi huyu ndiyo umesaidia
makampuni yake kuwekeza fedha kwenye mpira. Na mifano ipo hai tukianzia na
michuano ya Vijana ya Uhai Cup, ujenzi wa kituo cha michezo cha Chamazi ambacho
kinatumiwa na timu nyingi za Tanzania.
Na sasa tunafaidika na udhamini huu mnono ambao haujapata kutokea
katika historia ya Tanzania.
Tungependa viongozi wengi zaidi wa makampuni yanayoheshimika hapa
nchini wakijitokeza kuongoza mpira badala ya kuanza kuwapinga.
Kwa mfano, tungependa kuona mkurugenzi wa benki ya CRDB akiwa
kiongozi wa Ashanti, bosi wa Barrick akiongoza Mbeya City na Mkurugenzi wa
Tanga Cement akiongoza Coastal Union.
Hivi ndivyo namna mpira unavyoweza kuvutia wawekezaji. Ndiyo maana
tulifurahi wakati Yusuf Manji, alipoomba uongozi Yanga.
Bado tunataraji kwamba naye atajitosa kuingiza fedha zake kwenye
ligi ya Tanzania (mpira) kama alivyofanya Bakhresa ambaye pamoja na kutumia
fedha zake Azam FC, bado ameamua kusaidia na timu nyingine kwa ujumla.
Tunapenda kumuahidi Yusuf Manji kwamba iwapo naye atataka kudhamini
Ligi Kuu iwe kibiashara au kiufadhili, sisi tutamuunga mkono na hatutajali
suala la mgongano wa maslahi.
UPOTEVU WA MAPATO
Wenzetu Yanga wamedai
kwamba kwa kuonyesha mechi kwenye televisheni, mapato yake ya mlangoni
yatapungua.
Hili pia halikufanyiwa
utafiti wa kutosha. Katika siku za karibuni, mechi zilizoingiza mapato makubwa
zaidi ya milangoni ni zile ambazo zilionyeshwa Live kwenye televisheni za ndani
na nje ya nchi.
Mifano ni mechi za watani
wa jadi msimu uliopita zilizoonyeshwa Live na SuperSport na mechi za Kombe la
Kagame zilizoonyeshwa wakati huo.
Hata mechi ya Taifa Stars
na Ivory Coast iliyoonyeshwa Live pia, ilijaza uwanja. Ulaya ambako karibu kila
familia inamiliki televisheni na umeme wa uhakika, bado watu wanajaa katika
viwanja vya soka.
Mpira kuonyeshwa kwenye
televisheni unaufanya utangazike zaidi na watu watake kuona. Kuna faida nyingi
za mpira kuonyeshwa kwenye televisheni kuliko hasara moja ya kufikirika ambayo
Yanga wanaiona.
Ingekuwa vema iwapo Yanga
wangetoa takwimu za kuonyesha ni kwa namna gani mechi kuonyeshwa kwenye
televisheni kuliwahi kupunguza mapato ya milangoni.
Kwa faida ya umma, mpira
kuwa kwenye televisheni kuna faida zifuatazo; jezi kuongezeka thamani na hivyo
kuvutia makampuni makubwa kutaka kudhamini klabu wakitumia fursa ya kutangaza
bidhaa zao, matangazo ya viwanjani (touchline fence) kuwa na thamani zaidi
ambapo kwa sasa vilabu havipati chochote, kuchochea michezo ya kubahatisha,
kutabiri matokeo na kupata habari kupitia simu za mkononi na hivyo vilabu
vitaanza kutengeneza fedha za kutosha.
Ulaya wamesonga mbele
kutokana na televisheni. Anayekataa mpira kuonyeshwa kwenye televisheni ni sawa
na mtu anayegoma kutumia mfumo wa digitali katika ulimwengu wa leo.
UWAZI KWENYE MCHAKATO WA
KUUZWA KWA HAKI ZA MATANGAZO
Yanga wameandika kwenye
taarifa yao rasmi eti hakukuwa na uwazi kwenye mchakato wa kuipata kampuni ya
kurusha matangazo ya Televisheni.
Sote tunajua kuwa vituo
vya televisheni vilivyopo nchini kama Star TV ambayo iliwahi kurusha mechi
kadhaa msimu uliopita vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi hiyo na TFF mara kadhaa
wamekuwa wakitangaza hilo kupitia idara ya Habari ya TFF.
TFF kwa mfano walikwenda
mbali kwa kuialika Supersports kuja kuonesha mechi bure kwa kilichokuwa
kikiitwa Super Week ili kuwashawishi waje kuwekeza na mara ya mwisho ni Yanga
hawa hawa walioongoza harakati za kuikataa Supersports kuonesha mechi bure
wakisema kuwa kama ni kuwavutia inatosha.
Katika mazingira kama
haya tunastaajabishwa na ukigeugeu wa Yanga leo kusema eti tenda haikuwekwa
wazi. Sote tunajua kuwa ni Super Sports pekee tuliokuwa tukiwategemea na
kuwashawishi ambao hawakuonesha kuhitaji kuja kuwekeza. Kwa nini leo tuikatae
Azam TV?
Yanga wanaposema eti
TFF/Kamati ya Ligi imeipa haki za matangazo kampuni ambayo haina ofisi wala
kituo cha televisheni kilicho hewani kwa sasa wanasahau kuwa huko nyuma TFF
iliwahi kuwapa haki za matangazo GTV ambao hawakuwa na ofisi wala kituo cha TV
na baada ya miezi michache walifungua ofisi zao na kuleta vingamuzi na kuaza
kurusha mechi zetu. Vilabu vilifaidi udhamini ule kabla ya ile kampuni
kufilisika. Kwa hiyo hii si mara ya kwanza kwa jambo hili kufanyika na kama
Azam TV hawataonesha mechi za ligi hiyo sisi kama vilabu haituhusu kwani ni
hasara yao.
Tunachowaomba Azam Media sisi kama vilabu ni
kuhakikisha wanatulipa pesa zetu kwa haraka ili zitusaidie kwenye
maandalizi,Tunawaomba Yanga wasichafue hali ya hewa kwa kuwa wao hawana shida
ya Pesa.
Sisi Umoja wa Vilabu 13
vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania tunapinga, kwa nguvu zote, madai ya Yanga
kwamba hatukushirikishwa kama vilabu kwenye mchakato huu.
Mfumo wa ugawanyaji wa
mapato tuliouchagua, tuliuchagua wenyewe bila kushurutishwa na yeyote na
tunadhani ndiyo mfumo unaotufaa kwa sasa hadi hapo ligi yetu itakapokuwa na
nguvu maana kwa sasa inaruhusiwa klabu kupata fedha mwanzoni kulingana na hali
halisi ya vilabu vyetu.
Tunawashauri wenzetu wa
Yanga waanze kuamini kwenye kitu kinachoitwa Uwajibikaji wa Pamoja (Collective
Responsibility). Mambo yanayoamuliwa kwenye vikao hayapaswi kupingwa nje ya
vikao.
Kama hoja ililetwa kwenye
vikao na ikazidiwa nguvu na hoja nyingine, hakuna sababu ya kuikataa kwa sababu
tu hukubaliani nayo. Mfumo wa kidemokrasia una kanuni moja kuu; Wengi Wape
Imetolewa na
Vilabu 13 vya Ligi Kuu ya
Tanzania
Simba SC, Azam FC,
Ashanti United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Mgambo JKT, JKT Oljoro, Rhino
Rangers, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Kagera
Sugar.
MWISHO