YANGA V COASTAL UNION KESHO:BRANDTS AMHOFIA BOBAN

KOCHA mkuu wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara Yanga Sc, Ernie Brandts ameonesha kuhofia mchezo wa ligi hiyo baina ya timu yake na Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ unaotarajiwa kupigwa kesho katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Aidha, kocha huyo amemtaja mshambuliaji wa timu hiyo Haruna Moshi ‘Boban’ (pichani) kama ni mmoja ya wachezaji wa kuchungwa katika mchezo wa kesho.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya timu hiyo, Brandts amesema mchezo wa kesho unatarajiwa kuwa mgumu tofauti na watu wanavyodhani kutokana na ukwekli kwamba Coastal imejipanga msimu huu kwa kusajili wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji.
“Utakuwa mchezo mgumu na usiotabirika kwani wapinzani wetu wamejipanga vizuri, pia wachezaji wake ni mahiri kuna huyu Haruna Moshi ni mchezaji mzuri namfahamu makali yake tangu akiwa Simba...pia wana wachezji wa kigeni nao ni wazuri hivyo ni lazima wachezaji wangu wawe makini nao,”alisema
Hata hivyo Brandts alisema amekipanga vizuri kikosi chake ili kiweze kushinda mchezo huo na kuondoka na pointi tatu kama ilivyokuwa kwa mchezo wao wa kwanza wa ligi hiyo dhidi ya Ashanti United.
Katika mchezo wa kwanza wa Ligi hiyo Yanga iliichapa Ashanti mabao 5-1, huku Coastal Union itashuka ikiwa na kumbukumbu ya kuwaadhibu maafande wa JKT Oljoro kwa mabao 2-0.

Post a Comment

Previous Post Next Post