Na Onesmo Ngowi (Rais wa IBF Africa, Ghuba ya Uarabu na
Uajemi na mashariki na Kati )
Hivi karibuni Mtanzania Francis Cheka ambaye alikuwa bingwa wa IBF katika bara la Afrika uzito wa
kati (Super Middleweight) alimshinda bondia kutoka Marekani Phil William na
kutawazwa kuwa bingwa wa dunia anayetambuliwa na Shirikisho la Ngumi la Dunia
(WBF). Ushindi wa Cheka sio tu kwa Tanzania bali na kwa bara la Afrika na dunia
yote kwa ujumla.
Cheka ameungana na mabingwa wengine wa dunia wa uziro wa
kati (Super Middleweight) wanaotambuliwa na vyama na mashirikisho kadhaa kama
ifuatavyo:
IBF - Carl Froch kutoka nchini Uingereza
WBC - Andre Ward
kutoka nchini Marekani
WBA - Andre Ward
kutoka nchini Marekani
WBO - Robert
Stieglitz kutoka nchini Ujerumani
WBF - Francis Cheka
kutoka nchini Tanzania
IBO - Thomas Oosthuizen kutoka nchini Afrika ya
Kusini
Kwa uchache hao ni mabingwa wa uzito wa uzito wa kati (Super
Middleweight ) wanaotambuliwa na vyama/mashirikisho hayo niliyoyataja hapo juu.
Kati ya mabingwa wa dunia wa mashirikisho/vyama sita vikubwa duniani Afrika
imetoa mabindia wawili tu nao ni Francis Cheka kutoka nchini Tanzania na Thomas
Oosthuizen kutoka nchini Afrika ya Kusini.
Ubingwa alioupata Francis Cheka ni wa dunia na hautakiwi
upingwe na mtu yeyote yule nje ya ulingo bali wanaotaka kumpinga na kuukebehi
wanatakiwa wapande naye ulingoni au wamtafutie mtu wao apande naye ulingino ili
apigane na Francis Cheka.
Kwa bahati mbaya, taratibu na sheria za mchezo wa ngumi
haziruhusu mtu yeyote ambaye hayuko kwenye viwango vya ubora wa ngumi agombee
ubingwa wa aina yeyote ule.
Mashirikisho au vyama vya ngumi vimeweka utaratibu maalum wa
mabondia watakaoweza kugombea ubingwa wa dunia na mara nyingi ni wale tu walio
kwenye viwango vya juu kuanzia namba moja hadi namba tano.
Tanzania sasa tuna bingwa wa dunia katika uzito wa kati
(Super Middleweight) na ni Francis Cheka. Tunachukua fursa hii kumfagilia na
kumpongeza Francis Cheka kwa kulitangaza vyema jina la Tanzania na kuliweka
kwenye chati duniani.