Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amemjumuisha mchezaji Henry Joseph (pichani)wa Simba kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.
Tayari Joseph amesharipoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Taifa Stars ambayo iko chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29 mwaka huu, na leo jioni itafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. 
Programu ya timu hiyo inaonesha kuwa kesho (Septemba 3 mwaka huu) itafanya mazoezi yake asubuhi na jioni kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Karume. 
Wakati huo huo, kesho (Septemba 3 mwaka huu) saa 6 kamili mchana Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari.

LIUNDA KUTATHMINI WAAMUZI CL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa mtathmini wa waamuzi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Coton Sport ya Cameroon na Esperance ya Tunisia.
Mechi hiyo ya kundi B itachezwa Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Omnisport Roumdeadjia mjini Garoua, Cameroon. Kamishna atakuwa Bema Doumbia wa Ivory Coast.
Waamuzi wanatoka Madagascar wakiongozwa na Hamada Nampiandraza. Wasaidizi wake ni Jean Eric Pierre Andrivoavonjy, Ferdinand Velomanana Linoro na Bruno Marie Andrimiharisia.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)