CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)
kinatoa pongezi kwa bondia Francis Cheka kwa kuibuka bingwa mpya wa dunia wa
WBF katika uzito wa Super Middle.
Cheka alitwaa mkanda huo wa ubingwa baada ya kumshinda
Mmarekani, Phil Williams kwa pointi katika pambano la raundi 12, lililofanyika
kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam Ijumaa usiku.
TASWA imekunwa na mafanikio hayo na inatoa pongezi za dhati kwa
bondia huyo kwa juhudi zake na kulitangaza vyema jina la nchi yetu, hivyo
tunasema Cheka atambue familia ya wanamasumbwi na wanamichezo wote Tanzania
tumefurahishwa na mafanikio hayo na tunayajali.