STARS WAFANYIWE NINI ZAIDI YA HAYA YA TBL?


Na Dina Ismail, Tanzania Daima
KILIO cha wadau wa soka ni kushuka kwa kiwango cha soka cha Tanzania kunakotokana na kufanya vibaya kwa timu ya taifa, Taifa Stars katika kampeni za kucheza fainali za Afrika na Kombe la Dunia. 
Stars chini ya kocha Kim Poulsen iliyokuwa  ikipigania tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Brazil, imeishia njiani. 
Ikiwa katika Kundi C, Stars imemaliza kampeni Septemba 7 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kuambulia pointi sita katika mechi sita ilizocheza dhidi ya Ivory Coast iliyomaliza kinara, Morocco na Gambia. 
Wakati Stars ikiambulia pointi sita, Ivory Coast imemaliza na pointi 14 ikifuatiwa na Morocco pointi tisa huku Gambia ikimaliza ya mwisho baada ya kujitwalia pointi nne.

SAFARI YA STARS BRAZIL: 
Stars ilianza kampeni ya Brazil kwa kucheza na Chad katika mtoano wa kuwania kuingia hatua ya makundi. 
Ilianza kuwafuata Chad nyumbani kwao N’Djamena Novemba 11, 2011 ambako walishinda 2-1, na waliporudiana Uwanja wa Taifa, Dar ves Salaam Novemba 15 mwaka huo walifungwa 1-0, lakini wakasonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2. 
Matokeo hayo yakaifanya Stars kuingia kwenye kampeni hizo rasmi za kwenda Brazi ikipangwa kundi C, na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia. 
Stars ilianza kampeni yake Juni 2, 2012 kwa kuifuata Ivory Coast mjini Abidjan na kufungwa mabao 2-0, kisha Juni 10, 2012 ikarejea Uwanja wa Taifa kuisubiri Gambia na kuifunga mabao 2-1. 
Machi 24, 2013, ikawakaribisha Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, na kushinda 3-1. 
Hata hivyo, Morocco wakiikaribisha Stars mjini Marrakesh Juni 8, 2013, waliutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kwa ushindi wa mabao 2-1. 
Wakitoka kufungwa na Morocco, Stars walirejea nchini kujiandaa kuwakabili Ivory Coast na kuchapwa 4-2. 
Kipigo kutoka kwa Ivory Coast, ndicho kilizima ndoto ya Stars kuingia hatua ya mwisho ya timu 10 bora kuwania nafasi tano za kwenda Brazil kwa bara la Afrika. 
Hiyo ni baada ya kipigo cha Stars kuiwezesha Ivory Coast  kufikisha pointi 13 ambazo zisingefikiwa na nyingine kwenye kundi hilo, hivyo mechi za mwisho kuwa za kusaka heshima tu kwa Morocco, Tanzania na Gambia. 
Septemba 7, Stars wakicheza mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya Gambia, walifungwa mabao 2-0, mjini Bakau, matokeo ambayo kwa kiasi kikubwa yamewavunja moyo Watanzania. 
Wengi wao wanajiuliza tatizo hasa ni nini kwa timu hiyo? Ni udhaifu wa benchi la ufundi chini ya Poulsen? Ni aina ya wachezaji waliomo kwenye kikosi hicho au kukosa maandalizi bora yanayohitajika kulingana na ugumu na uzito wa kampeni hizo? 
Kufanya huko vibaya, Stars imezidi kuporomoka kwenye viwango vya soka duniani. Sasa inashika nafasi ya 127, licha ya kuwahi kupanda hadi  nafasi ya 89, mwaka 2007.

VIWANGO: 
Nafasi ya Tanzania kwa ubora wa soka katika miaka mingine ni kama ifuatavyo: 2012 (130), 2011 (137), 2010 (116), 2009 (106),  2008 (99),  2007 (89), 2006 (110), 2005 (165), 2004 (172), 2003 (159) na 2002 (153). 
Mwaka 2001 (149), 2000 (140), 1999 (128), 1998 (118), 1997 (96), 1996 (89), 1995 (70), 1994 (74) na 1993 Tanzania ilishika nafasi ya 98. 
Ndani ya 2013, kiwango cha Stars kimekuwa kibadilika kama rangi za kinyonga, Januari nafasi ya 124, Februari (127), Machi (119), April (116), Mei (116), Juni (109), Julai (121), Agosti 128 na Septemba (128). 
Matokeo ya uwanjani na mwenendo wa Stars katika viwango vya soka ulimwenguni, vimekuwa ni kinyume na matarajio ya wapenzi na wadau wa soka nchini.

UDHAMINI: 
Kabla ya mwaka 2006, moja ya sababu za kufanya vibaya kwa Stars katika medani ya kimataifa kwa maana ya kampeni za Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia, ni maandalizi duni kiasi cha kushindwa kuhimili kishindo. 
Fikra za wengi zikajielekeza kuwa pamoja na changamoto nyingine kama kutokuwepo kwa mfumo bora wa ukuzaji wa vipaji vya vijana, udhamini kwa Stars ulionekana kama ungeiwezesha timu hiyo kufanya vizuri. 
Ilitazamiwa iwe hivyo kwa vile wakati timu hiyo ikicheza bila udhamini, wachezaji walikuwa wakikusanywa na kufanya mazoezi ya pamoja kwa siku chache tu kabla ya mechi ya kimataifa kwa lengo la kukwepa gharama. 
Mazingira ya wakati huo yalikuwa magumu sana kiasi cha mchezaji kuona kuitwa Stars kama adhabu, hivyo kutoa visingizio kadha wa kadha vya kukwepa kujiunga na timu hiyo na walioripoti, hawakucheza kwa ari. 
Nani asiyekumbuka baadhi ya wachezaji hasa wa timu kubwa za Simba, Yanga na Mtibwa Sugar wakati huo, waliposingizia hili na lile ikiwemo ugonjwa au kuumia ikiwemo kujifunga bandeji ili kukwepa kuitwa Stars? 
Lakini, kuanzia mwaka 2006 chini ya utawala serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, hamasa ya kiongozi huyo katika maendeleo ya michezo ikaonekana kwa kuamua kumleta na kumlipa Kocha wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo. 
Mbali ya Maximo, pia Stars ikapata udhamini mnono wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) pamoja na Benki ya NMB, hivyo wachezaji na viongozi wa timu hiyo kuanza kufurahia uwepo wao katika timu hiyo. 
Ikiwa chini ya udhamini huo, Stars ikaingia katika vita ya kupigania tiketi ya fainali za Afrika za mwaka 2008 nchini Ghana, ikipangwa kundi la saba, ilimaliza kampeni nafasi ya tatu ikivuna pointi nane, nyuma ya Senegal (11) na Msumbiji (9) huku Burkina Faso ikiburuza mkia kwa pointi nne. 
Kwa kushindwa kwenda Ghana, Stars ikaelekeza nguvu katika mbio za kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani (CHAN), ambazo kwa mara ya kwanza zilichezwa nchini Ivory Coast. 
Stars chini ya Maximo, ikawa miongoni mwa miamba nane iliyocheza michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huo kuanzia Februari 22 hadi Machi 8. 
Katika kundi lake la A, Stars ilimaliza nafasi ya tatu ikijikusanyia pointi nne nyuma ya Zambia (5) na Senegal (5) huku wenyeji Ivory Coast wakiwa nafasi ya nne kwa pointi 1. 
Katika kundi B, Ghana ilimaliza kinara kwa pointi tano ikifuatiwa na DR  Congo (4), Zimbabwe (3) na Libya. DR Congo ilifanikiwa kubeba ubingwa. 
Stars kwa mara nyingine ikiwa chini ya Maximo, ikashiriki kampeni ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini na Kombe la Mataifa Afrika nchini Angola mwaka 2010. 
Ikipangwa katika kundi la D, Stars ilimaliza nafasi ya nne ikiwa ya mwisho kwa pointi 5, ikitanguliwa na Morocco (11), Afrika ya Kati na Algeria (8).

STARS BAADA YA MAXIMO: 
Stars ikaingia katika kampeni ya kucheza fainali za Afrika mwaka 2012, nchini Gabon na Guinea ya Ikweta, ikiangukia kundi D, ambako ilimaliza ya mwisho kwa pointi tano ikitanguliwa na kinara Morocco (11), Afrika ya Kati (8) na Algeria (5). 
Kwa kuepuka fainali za Afrika kugongana na Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, fainali hizo zikapangwa kuchezwa mapema mwaka huu nchini  Afrika Kusini huku Stars ilikosa tena tiketi chini ya Kocha Kim Poulsen.

NINI TATIZO? 
Msingi wa swali hili ni mazingira halisi ya sasa ya Stars kuwa tofauti na ilivyokuwa zamani (kabla ya 2006), kutokana na uwepo wa wadhamini kuanzia SBL na NMB hadi Kampuni ya Bia Tanzania (TBL). 
Baada ya kwisha kwa mkataba wa SBL na NMB, kuanzia Mei 9, mwaka 2012, Stars imekuwa chini ya TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager kwa udhamini wenye thamani ya shilingi bil 23 kwa miaka mitano. 
Ikiwa ni mwaka na miezi kadhaa, matunda ya udhamini huo ni makubwa kutokana na maandalizi na matunzo bora tenha ya uhakika kwa timu hiyo wakati wa kujiandaa na mechi ya kimataifa iwe ya ushindani au ya kirafiki. 
Mbali ya matunzo hayo, Stars wamepewa basi jipya lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 250, suti ya kisasa kwa kila mchezaji na kiongozi huku wasifu wa nyota tisa ukihifadhiwa kwenye DVD. 
Aidha, chini ya udhamini huo mnono, posho za wachezaji na viongozi sio tu zinalipwa kwa wakati, pia zimepanda kwa ujumla wachezaji wana uhakika wa yenye hadhi kiasi cha kila mchezaji kuona fahari kuitwa Stars. 
Vyote hivyo vimeongeza hadhi na thamani ya timu  hiyo kuanzia benchi la ufundi chini ya Kim, madaktari hadi wahudumu wa timu hiyo. 
Kwa wachezaji, mazingira bora yanawafanya kila mmoja wakiwmo chipukizi kutamani kuitwa kutimiza ndoto yao ya kutoa mchango wao kwa timu hiyo. 
Lakini, uwekezaji huo uliofanywa tangu, timu hiyo haijawa na uhakika wa kupata matokeo mazuri kiasi cha kucheza fainali za Kombe la Dunia wala zile za Afrika ambazo mara ya kwanza na mwisho ni mwaka 1980.

KAULI YA WADHAMINI

Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe anasema pamoja na kusuasua kwa timu hiyo katika medani ya kimataifa, wanajua mafanikio ya soka hayawezi kuja haraka kama wengi wangetamani iwe. 
Kavishe anasema wao wadhamini bado wana nia njema ya kuendelea kuidhamini Stars na kwamba ni matarajio yao timu itaendelea kuimarika siku hadi siku. 
Anasema jambo linalotia moyo zaidi wadhamini ni kuona wananchi bado wakiendelea kuisapoti timu yao wakionyesha imani kubwa, hivyo ni imani yao kuwa mafanikio yatapatikana tu. 
“Lengo hasa la mdhamini kwa sasa ni kuhakikisha Stars inafanikiwa kucheza  fainali za Kombe la Afrika za mwaka 2015,” anasema na kuwasihi Watanzania wasikatishwe tamaa na kushindwa kwenda Brazil. 
“Watanzania wasikate tamaa kwani mpira wa Tanzania ulikuwa bado, ni lazima kwenda hatu akwa hatua kama jinsi alivyoanza Kocha Kim Poulsen,” anasema Kavishe. 
Anasema wao wakiwa wadhamini wa timu hiyo, wanafarajika na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika Stars tangu waanze kuidhamini Mei 9, 2012.

WADAU: 
Baadhi ya wadau wametoa mawazo yao akiwemo nahodha wa zamani wa Stars na Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime anasema tatizo kubwa la wachezaji wa Stars ni kutojitambua, hivyo kutojua dhamana yao. 
“Tuwe wakweli, yaonyesha wachezaji wetu hawajitambui, wao ndio wanacheza soka uwanjani, hivyo wanapokuwa dimbani wanapaswa kupigania ushindi kwa nguvu na akili zote,” anasema Maxime aliyekuwa nahodha wa timu hiyo wakati wa Maximo na kuongeza: 
“Wakati wetu, tulikuwa tukiingia uwanjani tunajua nini tunatakiwa kufanya kwa mashabiki na nchi yetu, kwa sababu tunakuwa tumebeba dhamana ya Watanzania wote, tulihakikisha tunapambana, japo kufungwa ni sehemu ya mchezo.” 
Kuhusu benchi la ufundi chini ya Kim, Maxime anasema haoni tatizo na kamwe halipaswi kulaumiwa limekuwa likitimiza wajibu wake katika kuwaelekeza wachezaji wacheze vipi, hivyo wa kulaumiwa ni wachezaji. 
Mtazamo wa Maxime ni kama wa beki wa zamani wa Simba na Stars, Boniface Pawasa akisema tatizo kubwa ni wachezaji kukosa wivu na kiu ya kweli ya ushindi na mafanikio, hivyo wengi wao kucheza kwa kutimiza wajibu, hivyo timu ishinde, ifungwe au sare yote kwao ni sawa tu. 
Anasema chini ya mazingira hayo, ndio maana timu imekuwa kama homa ya vipindi, leo inacheza vizuri na kupata ushindi na kesho inacheza hovyo, hivyo hata ushindi wake huonekana kama ni kutokana na udhaifu wa timu pinzani. 
“Wachezaji wanapaswa kuwa na wivu na kiu ya ushindi vinavyobebwa na uzalendo katika kupigania ushindi uwanjani kwa kutambua kuwa watanzania wanataka ushindi kutoka kwao,” anasema Pawassa. 
Hata hivyo, Pawassa anasema kwa vile kuna uhusiano mkubwa kati ya Ligi Kuu na Stars, kuna haja ligi ikaboreshwa zaidi ili iweze kutoa nyota bora wa timu ya taifa. 
Pawassa anasema kinyume cha hapo, Stars itaendelea kufanya vibaya licha ya kuwepo kwa udhamini mnono zaidi katika historia ya soka chini ya uwekezaji mkubwa wa kampuni ya TBL. 
Anashauri uwekezaji uliofanywa kwa Stars, ufanyike pia kwa klabu za Ligi Kuu wanakotoka wachezaji wa kuunda timu hiyo kwani ligi mbovu pia hutoa wachezaji wabovu. 
Naye Steven Mapunda ‘Garrincha’ aliyewahi kuchezea Majimaji ya Songea, Simba na Stars, anasema kufanya vibaya kwa Stars kunatokana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kushindwa kutoka ofisini na kwenda kufanya mipango na fitna za ushindi. 
Garrincha anatoa mfano wa enzi ya Maximo, timu ilikuwa ikifanya vizuri kiasi kutokana na baadhi ya viongozi kuwa na mbinu mbalimbali ikiwemo ya nje ya uwanja kuiwezesha Stars kupata ushindi. 
“Viongozi wa TFF waache kukaa ofisini huko kazi yake ni kuandika taarifa na mambo mengine, soka ni mipango kwani kwa kushindwa kufanya hivyo, hata wachezaji wanajiona kama yatima tu hivyo wanacheza kwa kutimiza wajibu,” anasema na kuongeza: 
“Inasikitisha sana kwa timu yetu kufungwa hata na Uganda ambao hawana kikosi bora kama chetu….lakini wanatufunga tena tukiwa nyumbani, hii kwa kweli inatuumiza sana wadau wa soka.” 
Garrincha anakwenda mbali na kusema kama TFF wameshindwa kuisimamia, wangeikabidhi kwa viongozi wa Simba au Yanga waone itakuwa vipi kwa maslahi ya timu hiyo.

KIM POULSEN: 
Akizungumza baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa jijini Dar es Salaam (DIA) wakitokea nchini Gambia kucheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi na kuchapwa mabao 2-0, Kim alieleza mengi. 
Akiwa na wachezaji 18 waliokuwa kwenye msafara wa timu hiyo ambayo ilirejea nchini Septemba 9 (siku mbili baada ya mechi), Kim alisema moja ya sababu ya kufungwa, ni kuwakosa nyota wake muhimu wapatao tisa kutokana na kutoruhusiwa na klabu zao na wengine kuwa majeruhi. 
Poulsen anasema kutokana na hali halisi ya kikosi, alilazimika kupanga vijana wasio na uzoefu wa kutosha kuziba pengo la wazoefu kama Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu na wengine waliokosekana. 
“Tumesikitishwa na matokeo, lakini kama nilivyosema Gambia waliita wachezaji wao wote wanaocheza nje, sisi tulikosa karibia kikosi kizima cha kwanza...vijana waliocheza walijitahidi, lakini wenzetu waliwazidi uzoefu,” anasema. 
Anasema ni muhimu watanzania watambue kuwa mechi za kufuzu kucheza kombe la dunia zimekuwa muhimu sana kwa Tanzania kwani wachezaji wengi wametambulika na wameitwa nje. 
“Kuna wachezaji kama Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto ambao kutokana na mechi hizi wamepata nafasi ya kwenda kucheza nje,” anasema. 
Kocha huyo anasema yuko makini sana kutekeleza mpango wa muda mrefu ambao ni kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza Kombe la Afrika 2015 na kuongeza kuwa timu anayoendelea kujenga itafanya kazi hiyo. 
Anasisitiza kuwa ni lazima TFF ihakikishe wachezaji wote muhimu wanakuwepo wakati mechi za kufuzu kucheza Kombe la Afrika zitakapoanza mwakani. 
“Kwa sasa wachezaji watarudi vilabuni kwao na baada ya muda mfupinitawaita tena ili tujiandae na michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), yatakayofanyika Nairobi,” anasema.
Hata hivyo, anawasihi Watanzania wawe na subira kwani ana imani na timu anayoijenga.
“Tungefurahi kama tungefuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia, lakini ni mapema sana kwa timu yetu ambayo bado inajengwa…tumpe kocha nafasi aweze kutimiza haya malengo na sio kumkatisha tama,” anasema.

0788344566 dinazubeiry@gmail.com

Post a Comment

Previous Post Next Post