YANGA, SIMBA ZASHINDWA KUTAMBIANA, ZAGAWANA POINTI

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam/BONGOSTAZ BLOG
SIMBA SC leo imetoka nyuma kwa mabao 3-0 na kupata sare ya 3-3 na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Isarel Mujuni Nkongo, hadi mapumziko tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Mrisho Khalfan Ngassa alifunga bao la kwanza dakika ya 15 akimalizia kazi nzuri ya Didier Kavumbangu aliyepiga mpira wa juu uliomchanganya kipa Abbel Dhaira na kudondokea chini kabla ya mfungaji kuusukumia nyavuni.
Betram Mombeki alifunga la kwanza, SImba SC ikapata uhai na kurudisha yote

Simba SC ilikuja juu baada ya bao hilo na kujaribu kusaka bao la kusawazisha, lakini walikuwa ni Yanga tena waliofanikiwa kupata bao la pili dakika ya 36, mfungaji Hamisi Kiiza aliyeunganisha mpira wa kurushwa na Mbuyu Twite.
Bao la pili lilionekana kuwachanganya Simba na kuwaacha Yanga wacheze kwa madaha zaidi, pasi nyingi za aina zote na mbwembwe za kila aina.
‘Diego wa Kampala’, Hamisi Kiiza aliifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 45 akimalizia pasi nzuri ya Kavumbangu, ambaye aliipasua ngome ya Simba SC na kubaki na kipa Abbel Dhaira, lakini akaamua kumpa mwenzake amfunge Mganda mwenzake.  
Kipindi cha pili, mambo yalibadilika na Simba SC wakaanza kurudisha bao moja baada ya lingine hadi kupata sare ya 3-3.
Kocha wa Yanga Brandts akilia na wachezaji wake wakati Simba SC inarudisha mabao


Hamisi Kiiza alifunga mabao mawili kipindi cha kwanza

Alianza Betram Mombeki dakika ya 54 ambaye alipokea pasi nzuri ya Amisi Tambwe na kumtungua Ally Mustafa ‘Barthez’.
Yanga waliona kama Simba SC imepata bao la kufutia machozi, lakini kumbe kazi ndiyo ilikuwa inaanza na dakika ya 58 krosi maridadi ya Ramadhani Singano ‘Messi’ iliunganishwa nyavuni na beki Joseph Owino.
Bao hilo hakika liliwachanganya Yanga na wachezaji wa timu hiyo wakaanza kulaumiana wenyewe na kipa wao Barthez.
Lakini bado Simba SC iliendelea kutawala mchezo na Yanga SC walijaribu kufanya mashambulizi ya kupitia pembeni, ambayo yalidhibitiwa.
Mpira wa adhabu uliopigwa na Nassor Masoud ‘Chollo’ uliunganishwa kwa kichwa nyavuni na beki Kaze Gilbert kuipatia Simba SC bao la kusawazisha dakika ya 85.
Kwa ujumla, uhai wa Simba kipindi cha pili ulitokana na mabadiliko yaliyofanywa na kocha Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ kuwatoa Abdulhalim Humud na Haroun Chanongo na kuwaingiza Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’ mapema kipindi cha pili. 
Kwa Yanga SC iliathiriwa na kujiamini kwa wachezaji wake baada ya kwenda kupumzika wanaongoza mabao 3-0, lakini pia mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts kumtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Simon Msuva wakati wanaongoza 3-2 nayo yalipunguza kasi ya timu hiyo.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Haruna Chanongo/Said Ndemla dk48, Abdulhalim Humud/William Lucian ‘Gallas’ dk48, Betram Mombeki/Zahor Pazi dk90, Amisi Tambwe na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza/Simon Msuva dk61 na haruna Niyonzima. 

Post a Comment

Previous Post Next Post