SIMBA, YANGA ACHENI MAMBO YA KIZAMANI

Na Dina Ismail
IMEKUWA ni  mazoea kwa timu vigogo nchini, Simba na Yanga kutoa ‘kafara’ watu baada ya michezo baina yao.
Tabia hiyo imekuwa ikiota mizizi kadiri miaka inavyosonga ambapo kadhia hiyo huwakumba viongozi,wachezaji na wakati mwingine makocha.
‘Kafara’ hilo hufanywa zaidi kwa timu ambayo itakuwa imefungwa.
Hivi karibuni, Yanga iliachana na Mkurugenzi wake wa Ufundi, Mholanzi Hans Van Der Pluijim kwa madai ya kwamba inakabiliwa na ukata.
Pluijim alipata kuwa kocha mkuu wa Yanga kwa nyakati tofauti kabla ya mwaka jana mkataba wake kusitishwa tena baada  ya kutoka sare  ya bao 1-1 na Simba katika ambayo Yanga ilistahili kuibuka na ushindi.
Katika mechi hiyo ya msimu uliopita Yanga ilianza kufunga kupitia Hamis Tambwe, huku Simba ambayo ilicheza ikiwa pungufu baada ya nahodha wake Jonas Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu, ilisawazisha katika dakika za majeruhi kupitia kwa Siza Kichuya.
Hivyo matokeo hayo yali[pekea uongozi wa Yanga kumleta  kocha Mzambia George Lwandamina na hivyo Pluijim kuamua kusitisha mkataba wake.
Hata hivyo zilifanyika busara toka kwa wadau wa Yanga na hatimaye waliweza kumshawishi na kubaki kama Mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo.
Kutemwa kwa Pluijim kunakuja siku chache baada ya Yanga kupoteza mchezo wake dhidi ya mahasimu wao Simba baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara.
Hivyo basi, Yanga imeamua kumtoa Pluijim kafara kutokana na kipigo hicho na suala la ukata limewekwa kama ni sababu tu.
Inawezekana kweli Yanga wanakabiliwa na ukata kiasi cha kushindwa kumlipa Mholanzi huyo, lakini kwa kumtimua kipindi  baada ya kufungwa na Simba ni lazima tuamini kuwa ametolewa ‘kafara’.
Tukirejea historia za timu hizo zinapokutana lazima timu itakayofungwa kutatokea timuatimua au kusimamishwa kwa wachezaji au viongozi wa benchi la ufundi kwa madai kuwa walihujumu.
Kabla ya michezo baina yao huwa kuna tambo nyingi sana toka kwa kila pande huku kila mmoja akijinasibu ya kwamba yeye ni bora zaidi ya mwenzake.Sasa inakuwaje timu ikifungwa inadai kulikuwepo na hujuma?
Mpira una matokeo matatu;kufunga, kufungwa na kutoka sare, sasa Simba na Yanga kwa nini huwaga hamuamini matokeo ya kufungwa ambapo timu itayofungwa eti wamehujumu.
Hayo ni mambo ya kizamani na yaliyopitwa na wakati,haiwezekani kila mkutanapo timu ikifungwa mnahujumiwa.
Ikumbukwe kuwa mechi baina ya mahasimu kuna mambo mengi yanatokea, kuna kuzidiwa na mpira, kuna wachezaji kutokuwa vema kisaikolojia na mengineyo mengi hivyo ni wajibu kila upande kupokea matokeo yoyote itakayoyaopa.
Labda itokee suala la maamuzi ya uwanjani kuwa ya upendeleo wa wazi kwa timu moja na kupelekea ushindi hapo ndio mnaweza kuhoji lakini si kutimua ama kusimamisha wachezaji au viongozi pindi  timu inapiopoteza.
Ifikie mahala mbadilike na kuachana na mawazo ‘mgando’ yenu hayo kwani pia yanachangia kuwapoteza katika mechi zenu mingine.
Baada ya mechi kila timu ikubali matokeo na mambo mengine yaendelea na sio kukaa mnafanya uchunguzi nani chanzo cha kufungwa.

Yanga kumbukeni mna mchezo wa Ligi ya mabingwa hivi karibuni na pia mnaharakati za kutetea ubingwa, mkiendekeza kutafuta wa kumtoa ‘kafara’ mtajikuta mnapotea kila mahali.

Post a Comment

Previous Post Next Post