LIGI KUU ZANZIBAR 2024/25KUANZA SEPTEMBA 6

Na Mwajuma Juma,Zanzibar

LIGI Kuu ya Zanzibar kwa msimu wa 2024/2025 inatarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu.

Kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya mwaka huu, iliyotolewa na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), ligi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwakani.

Kalenda hiyo pia inaonesha kwamba zoezi la uhamisho na  usajili  limeanza kuanzia leo Agosti mosi na kumalizika Septemba 4, mwaka huum wakati Agosti 31 kutakuwa na mchezo wa ngao ya jamii.

Aidha kalenda hiyo inaonesha kwamba kabla ya kuanza kwa ligi hiyo kutakuwa na matukio mbali mbali likiwemo zoezi la utimamu wa mwili kwa waamuzi litakalofanyika Agosti 18 mwaka huu.

Zoezi hilo kwa mujibu wa kalenda hilo litaambatana na mafunzo kwa makocha pamoja na mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa shrikisho, klabu, mikoa na vyama.

Hata hivyo kalenda hiyo ambayo imeonesha matukio ya mwaka mzima pia ifikapo Disemba 15 hadi Januari 15 mwakani kipindi cha dirisha dogo la uhamisho na usajili, litakaokwenda sambamba na mashindano ya kombe la Mapinduzi.

Mnamo mwezi wa Disemba kwa mujibu wa kalenda hiyo kombe la Shirikisho FA mzunguuko wa kwanza kwa Unguja na Pemba na fainali yake itachezwa Mei mwakani.

Ligi kuu ya Zanzibar itashirikisha timu 16, ambazo ni JKU, Zimamoto, KMKM, KVZ, Uhamiaji, Mafunzo, Malindi, Mlandege, Chipukizi, Hard Rock, Kipanga, New City, Tekeleza, Junguni, Muembe Makumbi na Inter Zanzibar.


Post a Comment

Previous Post Next Post