MAFUNZO YA MCHEZO WA SHOTGAN ZANZIBAR KUFANYIKA AUGUST 8 & 9


CHAMA Cha Shotgan Zanzibar kinatarajia kufanya mafunzo ya mchezo huo yatakayofanyika nchini kuanzia Agosti 8 na 9 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mkufunzi Mkuu wa  mchezo huo Sense Abdalla Hussein Rashid alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alisema kuwa mafunzo hayo  yatafanyika katika uwanja wa Mao Zedong au New Amaan Complex kama utapatikana na kushirikisha waalimu pamoja na wachezaji wa mchezo huo.

Alifahamisha kwamba lengo la mafunzo hayo ni kutaka  kuwaweka sawa wachezaji pamoja na waalimu hao kukumbushana baadhi ya matukio ambayo yamo katika mchezo huo, pamoja na kujiandaa na mashindano ya mchezo huo yatakayofanyika Septemba 28 na 29 mwaka huu.

Hata hivyo alisema kuwa mara baada ya kufanyika mafunzo hayo washiriki wote watapata vyeti ambavyo vinatambulika kimatiafa.

“Ni mafunzo ambayo yanatambulika kimataifa na washiriki baada ya kumaliza watapatiwa vyeti vitakavyokuwa na uwezo wa kutumika popote pale ndani ya ardhi ya Afrika na Ulaya kwa ujumla”, alisema.

 Alisema kuwa hayo yataendeshwa na mkufunzi kutoka Afrika Kusini na yatashirikisha washiriki kati ya 20 na 30.

Post a Comment

Previous Post Next Post