ASKOFU BOAZ
Soko la muziki wa Injili linaendelea kukua na kupanuka siku hadi siku.
Inawezekana kukua na kupanuka huko kunatokana na mambo mengi lakini kubwa kuliko yote ni uungwaji mkono wa waimbaji wa Tanzania na wadau wa muziki huo.
Miongoni mwa waimbaji wanaofanya vizuri hivi sasa ni pamoja na Askofu Boaz Sollo ambaye licha ya kuwa askofu wa kutunza makanisa lakini amekuwa akitumia muda mchache wa ziada anaupata kumuimbia Mungu.
Hatua hiyo imemfanya kuwa na majukumu mengi zaidi katika kazi zake za kila siku hasa ikizingatiwa kuwa uimbaji ni kazi ambayo inahitaji muda na kutembea sehemu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa injili inawafikia wengi.
Askofu Boaz Sollo anasema kuwa katika kumtumikia mungu kuna talanta au karama ambazo kila mtu amepewa kwa namna hiyo hata yeye ameitwa katika mazingira tofauti walivyoiitwa waimbaji au watumishi wengine.
“Kimsingi binadamu hatujafanana ndiyo maana hata katika kumtumikia Mungu kila mmoja amekuwa amepewa karama tofauti nna ilivyo mtu mwingine.
“Nasema haya kwa sababu mimi ni tofauti na Bonny Mwaitege au Solomon Mukubwa ndiyo maana nasisitiza kuwa kinachohitajika ni kujua kuwa umeitwa kwa namna gani,” anaongeza Askofu huyo.
Kwa sasa Baoz Sollo ameshatoka na albam ya kwanza iitwayo Dhambi ni Mbaya Sana yenye jumla ya nyimbo tisa ndani yake ambayo ilizinduliwa hivi karibuni katika Ukumbi wa Hoteli ya Landmark jijini Dar es Salaam ambapo baadhi ya waimbaji wakiwemo Bahati Bukuku, Bonny Mwaitege, Sifa John pamoja na wengine wengi ambao wanafanya vizuri katika muziki wa Injili Afrika Mashariki walisindikiza.
Anasema uzinduzi huo pia utaambatana na uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kuanzishwa kwa kituo cha redio ya kikristo mjini Iringa.
“Katika shughuli hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam atakuwa ni mgeni wa heshima ambaye atasaidiana na mgeni rasmi katika kuchangsiha fedha na uzinduzi huo,” ameongeza Baoz.
Mbali na hilo, Boaz anasema uzinduzi huo utakuwa ni sehemu ya kuwasaidia watu wenye matatizo mbalimbali katika jamii ya Watanzania kwa maana pamoja na kuindua na kuchangisha fedha za uanzishaji wa kituo cha redio lakini watu wenye mahitaji muhimu katika jamii kama wagonjwa, yatima na wajane watakumbukwa kwa kupatiwa misaada.
" hii ni sehmu moja wapo ya kuwakumbuka wenye matatizo kwani wengi wa wanajamii wamekuwa wakijisahau hivyo kufanyika kwa uzinduzi huu itakuwa ni sehemu ya kuwakumbusha watu wengine wenye uwezo kujitoa kwa ajili ya wenzao wasiokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi”, aliongeza Boaz.
“Binafsi ni mtu ninayeamini kwamba jamii inahitaji mshikano na wa kweli ili kuweza kubadilika, natambua kwamba kwa kufanya hivi itakuwa ni sehemu muhimu na nyeti katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anajiona anajukumu la kuifanya nchi kuwa katika mabadiliko ya kweli,” anaongeza Askofu huyo.