MWENYEKITI WA YANGA LLOYD NCHUNGA
WALIOKUWA wagombea wa nafasi ya mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Francis Kifukwe na Mbaraka Igangula, wameombwa kuwa wajumbe wa bodi ya udhamini ya klabu hiyo.
Uteuzi huo umekuja siku chache baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa klabu hiyo ambao uliisha kwa Lloyd Nchunga kushinda kwa kura 1,437, akifuatiwa na Kifukwe aliyepata kura 370 huku Igangula akipata kura kura 305.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jana zilisema uamuzi huo umefikiwa na uongozi mpya kwa lengo la kudumisha umoja na mshikamano katika klabu hiyo kwa masilahi Yanga.
Kwa upande wa Kifukwe, tayari jana alipata barua ya kuombwa kuteuliwa kwa ajili ya kushirikiana na wajumbe wengine wa bodi hiyo, Yusuf Manji na Bi Fatma Karume.
Kupitia barua iliyokwenda kwa Kifukwe (nakala yake tunayo), Nchunga anamjulisha mhusika na kutakiwa kutoa jibu mapema kabla ya kamati ya utendaji kuketi leo kwa maamuzi rasmi.
KIFUKWE
Kwa maamuzi hayo, mdhamini wa klabu hiyo, Yusufu Manji, amemwandikia barua Kifukwe akimwomba akubali uteuzi huo wa Nchunga kuhakikisha Yanga inafanikiwa katika malengo yake ya kisoka na kiuchumi.
Kwa mujibu wa barua ya Julai 21, Manji amemwambia Kifukwe kuwa kazi ya udhamini wa Klabu ya Yanga ni ngumu, hivyo uteuzi wake utarahisisha kazi hiyo na kusema atafurahia kama watafanya kazi pamoja tena katika klabu hiyo.
Kuhusu Igangula, licha ya kuwepo kwa habari kuwa naye ameteuliwa, hadi kufikia jana mchana, bado alikuwa hajapata barua rasmi ingawa chanzo kimoja kutoka ndani ya uongozi huo mpya kimethibitisha kuwa Igangula naye amependekezwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Igangula tayari alishapigiwa simu na kuulizwa kama anaafiki uteuzi huo au la, naye akaridhia, lakini hadi kufikia jana mchana alikuwa hajapata barua rasmi kama ilivyo kwa Kifukwe.
Wakati tunakwenda mitamboni, Tanzania Daima ilimtafuta Igangula kwa njia ya simu kuhusu hilo na akasema hadi muda huo hakuwa ameipata, lakini akisema ni kweli juzi na jana alipigiwa na kiongozi mmoja wa klabu hiyo kujulishwa suala hilo.
IGANGULA
“Jana (juzi) na leo (jana), nilipigiwa simu na kuulizwa kama nipo tayari kuteuliwa kwenye Bodi ya wadhamini, nami sikuwa na sababu ya kukataa kwa masilahi ya Yanga, lakini barua rasmi haijanifikia, pengine ipo njiani,” alisema Igangula.