MJUE ‘TANZANITE’:MSANII AMBAYE WIMBO WAKE UMEPIGWA STOP, KISA KAUNAKILI KWA DIAMOND


TANZANITE
IMEZOELEKA Tanzania wimbo ukizuiwa kupigwa kwenye vituo vya redio au televisheni, ni kwa sababu umeimbwa kinyume cha maadili ya taifa letu, una lugha chafu au vinginevyo.


Lakini sasa mambo yanaanza kubadilika na umuhimu wa wasanii kusajili kazi zao Chama cha Haki Miliki na Haki Shiriki Tanzania (COSOTA) unaanza kuonekana, kwani wasanii wanakuwa wakali na kazi zao, kiasi kwamba kuzichezea sasa ni ngumu.

Wimbo ‘Kafara’ unajenga mfano wa nyimbo za kuwekewa pingamizi sambamba na kuweka rekodi ya kuwa wimbo wa kwanza kuzuiwa kuchezwa kwenye vituo vya redio na televisheni nchini, kwa sababu umelalamikiwa na msanii Nassib Abdul, maarufu kama Diamond.

Wimbo huo ulioimbwa na kijana anayechipukia kwenye Bongo Fleva, Mwingereza Athumani Mwingereza anayekwenda kwa jina la usanii la Tanzanite, umelalamikiwa na Diamond kwamba umenyofolewa kutoka wimbo wake wa ‘Mbagala’.

Diamond alipeleka mashitaka COSOTA dhidi ya Tanzanite ambaye anajulikana kwa jina la Abuu Fleva, akidai ameibiwa wimbo wake, hivyo kutaka sheria za haki miliki zichukue mkondo wake. Lakini pamoja na tuhuma hizo




za Diamond, mwanamuziki bora wa kiume Tanzania, Tanzanite amezama ndani na kumjibu hasimu wake huyo.

Katika mahojiano na Sayari wiki iliyopita, Tanzanite anasema kwamba Diamond amemgeuka, kwa sababu kabla hajatoa wimbo huo, alimtaarifu na wakakubaliana aurekodi.

“Nashangaa Diamond ameenda kushitaki COSOTA wakati kabla hata sijaurekodi nilimtaarifu wazo langu na alikubali…cha ajabu baada ya kuona wimbo umetoka na kukubalika zaidi ya wimbo wake ndiyo akaanza kuleta maneno, mara nimemwibia, mara ananishitaki na matokeo yake ndiyo ikawa hivyo ilivyotokea,” anasema.

“Sikuwa na dhamira ya kuimba remix ya wimbo huo, kuna siku ulikuwa unapigwa ‘Mbagala’ na mimi nikawa nafuata beats (ala zake) na kuweka maneno yangu, ndipo kuna mtu wangu fulani akanipa wazo la kuufanyia remix, nilimpigia simu Diamond, alikubali na nikatinga studio za Mahome na kufanya kitu ‘Kafara’,”’anasema.

Akifafanua zaidi, Tanzanite anasema kuwa mwenzake huyo amefikia hatua hiyo kutokana na kumhofia, kwani ni wengi wamekuwa wakizifanyia remix nyimbo za watu na zikatoka bomba zaidi ya zile za mwanzo, lakini hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa msanii aliyeuimba mwanzo (mmiliki).

Anasema kitendo alichokifanya Diamond si cha kiungwana wala kistaarabu hata kidogo, kwani awali alimkubalia na baadaye kugeuka, kisa kuona wimbo umepokewa vizuri, hivyo kutaka kummaliza kisanii kitu ambacho si rahisi kwani ana kipaji cha hali ya juu.

“Jamaa alianza chokochoko muda mrefu, hata jina hili alisema nimemuiga wakati mimi nilianza kulitumia tangu mwaka 2003, lakini kutokana na kazi zangu kutopata nafasi ya kutangazwa wala kurushwa hewani, leo hii nimeanza kufahamika kidogo anadai nimemuiga na jina, inashangaza sana,” anasema Tanzanite.

Akizungumzia hatua ya wimbo wake huo kupigwa marufuku, alisema haijamuathiri chochote kwani ana kipaji kikubwa katika medani ya muziki, hivyo hivi karibuni watu watamfahamu zaidi kupitia kazi zake alizozitayarisha.

Anasema amejipanga kikamilifu katika kuhakikisha anapanda meli ya wasanii wenye mafanikio na gumzo kutokana na ubora wa kazi zao na zenye ujumbe mzito kwa jamii, ambazo hazitawafanya wadau na mashabiki wa muziki kwa ujumla kuzichoka.

“Nina nyimbo nyingi nzuri na sijajua niachie upi, lakini muda si mrefu natarajia kuachia kibao changu kipya ambacho huenda ikawa sehemu ya ujio wa albamu yangu ya kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa naweza kusema imekamilika,” anasema

Anasema katika albamu hiyo ambayo itajulikana kama ‘More Fire’, atawashirikisha wasanii mbalimbali sambamba na kutumia studio tofauti katika kuitayarisha, lengo ikiwa kuipa vionjo na ladha tofauti.



ALIKOTOKEA:

Alianza kuupenda muziki tangu akiwa mdogo na hasa alikuwa akivutiwa na wasanii waliokuwa wakiunda kundi la Daz Nundaz Family - hapo unawazungumzia akina Ferooz, Daz Baba, La Rhumba, Critical na Sajo. Lakini pia Dully Sykes na Mr Blue ni wasanii wengine waliomtia Tanzanite mizuka ya kujitosa kwenye ‘game’, kwani anasema kila alipokuwa akisikia nyimbo zao zilikuwa zikimtamanisha kufuata nyayo zao.

Lakini ilimuwia vigumu mwanzoni kujiingiza kwenye muziki, kutokana na familia yake kushika dini ya Kiislamu mno, hivyo kumzuia asifanye mambo hayo.

Lakini Tanzanite akawa mbishi, alianza kufanya kwa siri hatimaye ikaja kujulikana mtaa mzima kwamba kijana ni mwanamuziki na ana kipaji hivyo wazazi wakashindwa tena kumdhibiti.

Akizama ndani zaidi, anasema kutokana na kusoma elimu ya dini ya Kiislamu vizuri madrasa, kila alipokuwa akiingia msikiti kusali na kuona mic (kipaza sauti), alikuwa anapandisha mizuka na kutamani kwenda kuichukua ili ashushe mistari, lakini alikuwa anajizuia ili asiharibu ibada yake na za wengine.

“Baba yangu alitaka nisome shule zinazofundisha elimu ya Kiislamu, lakini kutokana na mimi kupenda mambo ya muziki niliamua kuondoka nyumbani ili nikafanye kitu ambacho roho yangu inapenda, huwezi amini sina mawasiliano mazuri na baba kutokana na mimi kujihusisha na muziki, yote kwa yote kutokana na kuwa nimedhamiria kufanya kitu fulani, hilo halinipi hofu naamini Mungu atanisaidia nitatimiza ndoto zangu,” anasema.

Katika safari yake ya kusaka mafanikio ya kimuziki, anasema kwamba mwanzoni alipata tabu kidogo kupata nafasi ya kurekodi nyimbo zake, lakini baada ya watayarishaji wengi wa muziki kubaini kipaji alichonacho, walianza kudata na yeye, hivyo kumpa nafasi.

Anakiri kwamba hivi sasa kuna ushindani wa hali ya juu kwenye soko la muziki wa Bongo Fleva kutokana na utitiri wa vipaji vinavyoibuka, lakini yeye anasema kwake hiyo ni changamoto ya kukomaa zaidi, ili ashinde vita hiyo na kuwa namba moja siku moja, ili wafunge midomo watu kama Diamond, anayetamba na albamu yake ya ‘Platinum’.

“Mimi nawashauri wasanii wenzangu wasiwadharau wasanii chipukizi, kwani hata wao kabla ya kufika hapo walipo, walianzia kwenye uchipukizi, hivyo wanatakiwa kuwaonyesha njia walizopitia na wao, ili kuwasaidia kuinuka kimuziki,” anawashauri magwiji wa Bongo Fleva.

Kabla ya kutoa wimbo wa ‘Kafara’, Tanzanite alitoa ‘Umejuaje’ mwaka 2008, aliomshirikisha Ney wa Mitego ambao hata hivyo ulibaniwa na ma-DJ wa vituo vya redio hivyo haukuwafikia wapenzi wa muziki.

3 Comments

  1. Huyu jamaa anatakiwa aanze upya kwa kubadilika kimtazamo na ajiamini kuwa anaweza ndiyo atafanikiwa. Anonekana yeye ni mtu wa kukopi tu kama wachina kwani hata jina "Tanzanite" unaona lilivyo na maana ya madini kama ambavyo tunaona "Diamond".
    Natoa ushauri kwa wasanii wote wawili kukaa na kuangalia namna ya kuufanya huo wimbo uendelee kupigwa kwa manufaa ya wote kwa usimamizi wa COSOTA. Naamini kabisa huyo kijana anamkubali sana Diamond na ndo maana akawa anamuiga kila kitu. Hivyo Diamond anatakiwa amchukulie kama wapenzi wake wakubwa ambao wanamfeel ile mbaya na amsamehe kwa kuukopi wimbo bila makubaliano, then waende COSOTA kufuta hiyo kesi. Naamini hata mauzo ya "Mbagala" lazima yameongezeka na pia umaarufu wa Diamond umeongezeka kwa mtu kuweza kuuiga wimbo wake kivile.

    Kwa hiyo wadogo zangu nafikiri mngekaa tu mkayaongea haya kwani yanajadilika haya. Mbona tumeweza kuwafahamu hata "Golden Sound" ambao hawakuwa maarufu kabisa kwa sababu ya wimbo wao Shakira alioucopy na kuufanya uwe wimbo bora wa FIFA? Ni ukweli kwamba kuna watu wengi sana wanatafuta album ya hao walioimba Zangalewa miaka kibao iliyopita na ilishasahaulika hata kwa wale waliowafahamu. Mie pia nautaka huo wimbo wa Golden sound.

    So guyz, take it easy and talk.

    ReplyDelete
  2. Aah we Tanzanite kwani ni lazima ukopi kazi ya mtu? Kama kweli una kipaji basi tunga nyimbo zako na beat zako sio za kukopi hata mimi nilipousikia huo wimbo wako wa KAFARA kwakweli sijapenda kabisa kwakuwa karibu maneno na mtiririko mzima wa wimbo wako umechukua kwa jamaa!!! Sio fresh Diamond ana haki kulalamika! Mtu kasugua kichwa wee unakuja una copy na ku paste! Noma!!!!

    ReplyDelete
  3. Tanzanite hilo la Diamond lisikutie hofu kwani wasiwasi wake kwa wewe ni kunyanyuka zaidi.Changamoto hilo ni njia ya wewe kuongeza juhudi katika kazi zako katika fani hii ya muziki. Kaza buti mwanamme na toa vibao vikali vitakavyowakomesha wasio na uhakika na miziki yao kama Diamond.Nakutakia mafanikio mema.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post