MENEJA WA BIA YA KILIMANJARO GEORGE KAVISHE AKIMKABIDHI JEZI MAKAMU MWENYEKITI WA SIMBA< GEOFREY NYANGE "KABURU'
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), jana ilitoa vifaa vya michezo kwa klabu za Simba na Yanga vyenye thamani ya sh mil. 64 kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu ya Bara itakayoanza Agosti 21 ikishindanisha timu 12.
Wakati mabingwa watetezi Simba wakianzia kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam dhidi ya African Lyon, Yanga siku hiyo watakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuwakabili maafande wa Polisi wa huko.
Akikabidhi vifaa hivyo jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema, udhamini wa Bia ya Kilimanjaro kwa timu hizo, ni sehemu ya mkakati wa kuzinufaisha timu hizo na soka la Tanzania kwa ujumla kufika katika kilele cha mafanikio.
“Udhamini huu ni sehemu ya mkakati wa bia ya Kilimanjaro kuona inalifikisha soka ya Tanzania katika kilele cha mafanikio kwani vifaa vilivyokabidhiwa vinatarajiwa kutumiwa na timu hizo katika mazoezi na mechi za Ligi Kuu,” alisema Kavishe.
Alisema utoaji wa vifaa hivyo, ni awamu ya kwanza kati ya mbili ndani ya msimu mmoja kwa mujibu wa mkataba wa udhamini ambao umekuwa pia ukihusisha vifaa vya michezo kwa awamu mbili za ligi, kulipa mishahara kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi ambapo mwaka jana ilizipatia timu hizo magari mawili kwa ajili ya safari za timu.
Kwa upande wa wawakilishi wa klabu hizo, waliishukuru TBL kwa udhamini huo na kuahidi kuvitumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Katika hafla hiyo Yanga, iliwakilishwa na Mwenyekiti wake mpya, Llyod Nchunga, ambaye alisema udhamini wa TBL ni sehemu ya urejeshaji wake faida kwa wananchi huku Simba wao wakiwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Godfrey Nyange Kaburu, ambaye aliahidi kuuenzi udhamini huo.