KUGOMA WIMBO WA TAIFA UWANJA WA UHURU, KAMATI YAMKAANGA KAIJAGE


FLORIAN KAIJAGE, ALIYEKUWA OFISA HABARI WA TFF
KAMATI ya Uchunguzi wa sakata la kugoma kupigwa nyimbo za taifa siku ya mchezo wa kimataifa kati ya Taifa Stars na Morocco Oktoba 9 mwaka jana, iliyoundwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, imemaliza kazi yake na kubainisha kuwa aliyekuwa Ofisa habari wa Shirikisho hilo Florian Kaijage alifanya uzembe.
Akitoa taarifa ya tume hiyo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamidu Mbwezeleni, alisema kuwa, kulikuwa na makosa madogo madogo, hasa likiwamo la Kaijage kutofanya majaribio ya CD za nyimbo hizo kabla ya tukio, ambazo zilikuwa mikononi mwake, sambamba na kutozifikisha kwa wakati uwanjani na kuthibitisha kama ni sahihi.
Kwa mujibu wa Mbwezeleni, kutokana na tatizo hilo, kamati inamshikilia Kaijage kuwa ndiye aliyesababisha kutopigwa nyimbo hizo kwa wakati mbele ya mgeni rasmi siku hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na kuwa hatua iliyochukuliwa dhidi yake ya kusimamishwa ilikuwa sahihi.
Alisema, Kaijage alipowasilisha CD hiyo kwa mhusika aliyetakiwa kupiga, ambaye ni raia wa China, alitakiwa kusubiri zifanyiwe majaribio kama zinastahili kutumika, jambo ambalo hakulifanya na mhusika huyo alishindwa kutafuta ufumbuzi baada ya kutomuona tena Kaijage katika eneo hilo.
Mbwezeleni alisema, kama Kaijage angesubiri CD ya mwanzo kuchezeshwa au angefanya mazoezi kabla na kuthibitisha ukamilifu wa CD ya mwanzo kwenye mashine, suala hilo lisingefikia lilipofikia.
“Zile CD, zilikuwa haziingiliani na zile mashine na katika kuhangaika kutatua tatizo, kuna mtu alijitokeza kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi, lakini ilishindikana kutokana na Mchina mhusika kutojua Kiingereza na Kiswahili, hivyo ilikuwa ngumu sana kutatua tatizo lile,” alisema Mbwezeleni.
Aidha alieleza, kamati ilibaini bila ya kificho kuwa, Oktoba 8 ndiyo siku ambayo umeme ulirejeshwa uwanjani, ambako haukuwepo takribani miezi miwili, huku akisisitiza kwamba, hata hivyo siku hiyo mchana Wachina wengine wahusika wa uwanjani hapo walikuwepo na yaliyokuwa ya lazima kufanyiwa marekebisho yalifanyiwa, isipokuwa Kaijage hakutokea eneo la tukio.
Alisema, Oktoba 9 ambyo ndiyo ilikuwa siku ya mechi baina ya Taifa Stars na Morocco, Kaijage katika maelezo yake alidai kuwa, alipata CD ya pili ya Morocco kutoka kwa wanadiplomasia wa nchi hiyo waliotoka Nairobi majira ya saa 4 asubuhi, hata hivyo yeye alifika uwanjani kwa mara ya kwanza majira ya saa 8 mchana, muda mfupi kabla ya shughuli kuanza, wakati haikuwa kweli, kwani alifika wakati shughuli zinaendelea.
Kamati hiyo ilitoa ushauri kwa TFF kuwa, taratibu ziwekwe ili mhusika wa kwenye studio hizo za uwanja huo awe ni Mtanzania au akiwa Mchina kama ilivyo hivi sasa, ni vema siku ya michezo awe studio saa moja kabla ya michezo bila kuondoka, ikiwamo watu wa utaratibu wa TFF kumpa nyimbo hizo za taifa kabla ya siku moja kwa ajili ya mazoezi.
Pia kamati hiyo ilishauri kwamba, suala la mazoezi ya vyombo na mashine za sauti liwe ni la lazima na watakaohusika suala hilo waandikwe.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, awali kabla ya mechi hiyo, Tenga alimwagiza Kaijage kuchukua CD hiyo ya wimbo wa taifa wa timu ya wageni mapema na kwenda uwanja wa taifa kufanya majaribio, ili kama kuna upungufu uweze kushughulikiwa mapema, ambako kutokana na tukio hilo la aibu, TFF iliomba rahi kwa Rais Kikwete na wageni kutoka Morocco na mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo.
Tenga aliunda kamati ya watu watano kwa ajili ya kuchunguza sakata hilo, chini ya mwenyekiti wake Mbwelezi na wajumbe Yusuf Nzowa, ACP Ahmed Msangi, Gasper Mwembezi na Zena Chande.

Post a Comment

Previous Post Next Post