MAHAKAMA YAMWACHIA HURU MWAKALEBELA


Na Francis Godwin, Iringa
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Iringa imemwachia huru, aliyekuwa mshindi wa kwanza katika kura za maoni katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fredrick Mwakalebela (41), ambaye alikuwa akikabiliwa na shitaka la kudaiwa kutoa rushwa wakati wa mbio za kuomba kuteuliwa kuwa mgombea ubunge kupitia chama hicho.
Wakati ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wa Mwakalebela ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kabla hajajitosa kwenye siasa, wakiondoka mahakamani hapo kwa furaha kubwa na kumzuia kuzungumza chochote na vyombo vya habari kwa madai Mungu ametenda kazi yake.
Awali akisoma shitaka hilo mbele ya hakimu, Festo Lwila, mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), Imani Mizizi alidai kuwa, Juni 20, mwaka jana mshitakiwa Mwakalebela alitoa hongo ya sh 100,000 kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, Hamis Luhanga ili awagawie wajumbe 30 wa CCM, ambao waliitwa kwenye kikao hicho cha kujipanga kushinda kura za maoni.
Mwanasheria huyo alidai kuwa, mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume kinyume cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007, kifungu cha 15(1),(b), kinachokwenda sambamba na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka mwaka 2010 kifungu namba 21 (1), (a) na kifungu cha 24(8).
Hata hivyo, hati ya mashitaka hayo iliwekewa pingamizi na wakili wa upande wa utetezi chini ya Basil Mkwata, ambaye aliwasilisha pingimizi la awali la kisheria, ukiomba kesi hiyo iondolewe mahakamani kutokana na mapungufu ya kisheria yaliyofanywa na upande wa mashitaka, ambao ni TAKUKURU.
Katika pingamizi hilo, wakili wa utetezi alisema, mshakiwa alishaadhibiwa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kumuengua katika uchaguzi wa kura za maoni, hivyo kuomba shtaka hilo liondolewe mahakamani.
Kesi hiyo ambayo ilionyesha kuwa na mvuto zaidi kwa wakazi wa Mkoa huu, ambao jana walifurika mahakamani hapo kutaka kujua hatma yake.
Hakimu wa mahakama hiyo, baada ya kusoma maelezo ya pande zote mbili kwa mapana zaidi, ndipo alipolazimika kuliondoa shauri hilo mahakamani, kwa madai halina uzito na kutaka TAKUKURU kuandaa mashtaka mengine, iwapo watataka kuendelea na kesi hiyo.
Hakimu huyo alisema kuwa, mahakama imeridhia pingamizi hilo kwamba, mshtakiwa alishtakiwa kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashitaka, kitu ambacho ni kinyume cha sheria na kinaweza kumsababisha ashindwe kuandaa utetezi wake, kwa kutojua lipi anakabiliana nalo.
Alisema kuwa, hakukuwa na sababu ya kuweka katika hati moja mashtaka mawili na kwamba, usahihi wa hati ya mashtaka unapaswa kuwa makini tangu awali unapoandaliwa, jambo ambalo limemfanya Mwakalebela kuwa huru.

Post a Comment

Previous Post Next Post