SUGU AWACHONGEA WASANII WENZAKE KWA WANANCHI, NI WALE WANAIPIGIA DEBE CCM


NA Janet Josiah, Musoma
MBUNGE wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr.II (CHADEMA) amewataka Watanzania kuwahukumu wasanii wa miziki hapa nchini ambao wamekuwa wakikipigia debe Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kutoingia kwenye matamasha yao.
Mbunge huyo amesema, wapo wasanii ambao wamekuwa wakiishabikia CCM kuwabeza wananchi na kwamba wasanii wa namna hiyo ambao wanafahamika wanapaswa kuhukumiwa kwa wananchi kutoingia katika maonyesho wanayoyafanya kwenye maeneo yao.
Mbilinyi aliyasema hayo juzi mjini Musoma mkoani Mara, wakati alipozungumza na halaiki ya watu waliojitokeza kwenye maandamano makubwa ya Chadema, yaliyofanyika katika viwanja vya Mkendo mjini hapa.
“Ndugu zangu wapo wasanii wanawasaliti wananchi kwa kukodiwa na CCM wakati wa kampeni...wasanii hawa msiwe mnaenda na kulipa kwenye matamasha ama maonesho yao.
“Kama wanakula meza moja na CCM ina maana hawawapendi Watanzania, hukumu yao ni ya kutokwenda wala kununua miziki yao, si mnawajua lakini?” alihoji Sugu ambaye aliwahi kutikisa anga la muziki miaka ya nyuma.
Aidha, mbunge huyo alisema wasanii wanaoshirikiana na CCM hawawatakii mema wananchi na kwamba watu hao ni sawa na wasaliti wakubwa, hivyo wanatakiwa wahukumiwe kwa staili ya kususiwa kazi zao.
Katika mkutano huo ambao ulifurika maelfu ya watu, Sugu ambaye aliitwa na wananchi kupanda jukwaani kuwapa mistari (kuwaimbia muziki), alihitimisha mkutano huo mkubwa kwa kuimba nyimbo zake kadhaa.

Post a Comment

Previous Post Next Post