TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIMei 4, 2011USAJILI KILI TAIFA CUP 2011
Kamati ya Mashindano ya TFF ilikutana jana ambapo pamoja na mambo mengine ilipitia maombi ya usajili kwa timu zinazoshiriki michuano ya Kombe la Taifa (Kili Taifa Cup 2011) inayoanza Mei 7 mwaka huu katika vituo sita vya Lindi, Mbeya,
Morogoro, Moshi, Mwanza na Tabora.
Usajili wa wachezaji wote umepitishwa isipokuwa wawili tu. Wachezaji hao ni Nurdin Mussa Mponda aliyeombewa usajili timu ya Mkoa wa Temeke na Kudura Hamis Maguta aliyeombewa Kinondoni.
Wachezaji hao waliombewa usajili kinyume na kanuni namba 33 ya michuano ya Kombe la Taifa.
Mponda msimu huu amechezea Villa Squad ya Kinondoni, hivyo hakuwa na sifa ya kuchezea timu ya Mkoa wa Temeke wakati Maguta alichezea Moro United ya Mkoa wa Ilala ingawa aliombewa usajili akioneshwa kuwa ni mchezaji wa Red Coast.
Ukiondoa Ligi Kuu, kanuni inataka wachezaji wa madaraja mengine wachezee mkoa ambao timu zao la ligi zimesajiliwa
SIFA ZA MAKOCHA
Kwa mujibu wa Kanuni ya 42 ya michuano hiyo, makocha wakuu wa timu za mikoa wanatakiwa kuwa na cheti cha ngazi pevu (Advance Level) wakati wasaidizi wanatakiwa kuwa na cheti cha ngazi ya kati (Intermediate Level).
Kamati imezikumbusha timu zote zinazoshiriki michuano hiyo kutokwenda kinyume na sifa hizo kwa vile tayari zina kanuni za mashindano ya Taifa 2011Ligi hiyo inayoshirikisha mabingwa wa mikoa imepangwa kuanza Juni 11 mwaka huu katika vituo vya Kigoma, Mbeya, Pwani na Singida ambavyo vilishatangazwa awali.
Usajili utafanyika kuanzia Mei 10 hadi 25 mwaka huu wakati kipindi cha pingamizi ni kuanzia Mei 26 hadi Juni 3 mwaka huu. Usajili utapitishwa Juni 4 mwaka huu wakati ada ya kushiriki ni sh. 70,000 na kadi ya mchezaji ni sh. 6,000 ambapo timu zinatakiwa kulipa wakati wa kurejesha fomu za usajili.
Mikoa ambayo imewasilisha rasmi TFF mabingwa wao ni Dodoma (Majengo FC), Kigoma (Kasulu United), Kilimanjaro (Lang’ata Bora FC), Morogoro (Tumbaku) na Mwanza (Geita Veterans).
Hivyo, Kamati imeagiza mikoa ambayo haijawasilisha majina ya mabingwa wao kufanya hivyo haraka, kwani ikishindwa ligi itaendelea kwa tarehe zilizopangwa bila timu zao kuwemo.
Vilevile mikoa ambayo imemaliza ligi zao, lakini bingwa hajapatikana kutokana na rufani, zimetakiwa kusikiliza rufani hizo haraka.
LIGI KUU YA VODACOM 2010/2011
amati imemfungia mechi tatu za ligi hiyo Daktari wa Yanga, Juma Sufiani baada ya kumsukuma mchezaji mmoja wa Azam kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Atatumikia adhabu hiyo kuanzia msimu ujao wa ligi. Mwamuzi wa mechi hiyo alimtoa kwenye benchi kutokana na kosa hilo.
Suala la mchua misuli wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein kumtukana mwamuzi msaidizi Saada Hussein, na lile la mshambuliaji wa timu hiyo Gaudence Mwaikimba kuwafuata waamuzi vyumbani na kuwatukana baada ya mechi dhidi ya AFC iliyochezwa Aprili 10 mwaka huu Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba yamepelekwa Kamati ya Nidhamu.
mujibu wa Kanuni, makosa yote ya kinidhamu yanayotokea nje ya uwanja adhabu zake zinatolewa na Kamati ya Nidhamu ambayo kwa sasa inaongozwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) mstaafu Alfred Tibaigana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari TFFM