Katika msafara huo wachezaji ni 19 huku benchi la ufundi likiwa watu wanne.
Kiongozi wa msafara ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) Lina Mhando ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Twiga Stars inashiriki michuano hiyo ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) ikiwa timu mwalikwa. Jumla ya timu nane zinashiriki wakiwemo wenyeji Zimbabwe.
Nyingine ni Lesotho, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi. Twiga ambayo iko kundi A pamoja na Zimbabwe, Lesotho na Botswana itacheza mechi yakeya kwanza Julai 2 mwaka huu dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Gwanzura.
Siku inayofuata itacheza na Lesotho kwenye Uwanja wa Rufaro kabla ya kumaliza mechi za makundi Julai 5 mwaka huu kwa mechi dhidi ya wenyeji kwenye Uwanja wa Gwanzura.
Hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itafanyika Julai 7 mwaka huu.
Kila kundi linatoa timu mbili kuingia katika hatua hiyo na nusu fainali zote pamoja na fainali zitachezwa Uwanja wa Rufaro.
Boniface Wambura
Ofisa Habari-TFF