KIINGILIO cha juu katika mchezo wa fainali za Kagame Castle Cup, itakayowashirikisha Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara, Yanga na Simba ni shilingi 30,000 kwa VIP A wakati kiingilio cha chini ni sh 3000 kwa jukwaa la kijani.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah VIP B ni shilingi 20,000, VIP C ni shilingi 10,000, rangi ya chungwa mzunguko na nyuma ya magoli ni shilingi 7,000 na bluu shilingi 5000.
Osiah alisema viingilio hivyo ni kwa michezo miwili, fainali na mchezo wa kuwania mshindi wa tatu utakaochezwa saa saba na nusu mchana.
Aidha Osiah alitoa wito kwa mashabiki kununua tiketi kwenye vituo vinavyouza tiketi ambavyo ni sekondari ya Benjamin Mkapa, Bigbon Kariakoo, Steers, Mlimani City na baadaye uwanja wa Taifa.
Osiah alisema mashabiki wasinunue tiketi kwa washika mkononi walio karibu na vituo na magari yanayouza na badala yake wanunue kwenye vituo husika.
Alitoa wito kwa mashabiki kuzingatia ustaarabu waingiapo uwanjani hasa kwa viti na kutotoa lugha chafu sambamba na usafi uwanjani hapo.
“Suala la ulinzi limekamilika kwa kiasi kikubwa, hivyo mashabiki wasisite kuja na magari yao uwanjani hapo, kwani hata katika kambi za jeshi zilizopo karibu na uwanja zina maegesho ambayo yanatumika,” alisema Osiah.