UONGOZI wa klanu ya soka ya Simba unatarajia kuwakabidhi barua wachezaji waliotolewa kwa mkopo kwenye klabu nyingine za Ligi Kuu Tanzania bara ili waeleze sababu za kusambaza taarifa kupitia vyombo vya habari zinazoonyesha kulumbana na uongozi ikiwa wao hawajawaacha.
Kamwaga alisema sababu ya kupeleka barua kwa wachezaji hao ni muonekano wa malumbano baina ya wachezaji na viongozi jambo ambalo ni kanuni ya mashindano na si matakwa yao sambamba na taratibu za benchi la ufundi.
“Wachezaji tuliowapeleka klabu nyingine kwa mkopo inatakiwa wakakuze viwango vyao baada ya kuonekana kupoteza uwezo wao, kwani bado ni wachezaji halali wa Simba, ikiwa tutawahitaji watarejea kwetu,” alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema kuporomoka kwa viwango vya wachezaji hao kumeonekana kupitia mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA, Kagame Cup’ yaliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa Simba waliopelekwa kwa mkopo ni pamoja na Mohamed Banka, Mohamed Kijuso, Haruna Shamte (Villa Squad), Aziz Gilla (Coastal Union) na Meshack Abel (Ruvu Shooting).