CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), kinasikitika kutangaza kifo cha mwandishi mahiri wa habari za michezo Zanzibar, Maulid Hamad Maulid.
Maulid ambaye anafanyia kazi vituo vya Redio One na ITV akiwa Zanzibar, amefariki dunia leo Jumanne Oktoba 18, 2011 asubuhi nyumbani kwake Jang’ombe Zanzibar.
Taswa imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Maulid kwani alikuwa kiungo muhimu kwa ushirikiano kati ya Taswa na waandishi wa habari za michezo Zanzibar.
Pia Maulid alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Taswa Zanzibar ambayo ilianzishwa hivi karibuni kwa lengo la kuwaweka pamoja waandishi wa habari za michezo Zanzibar.
Tumepoteza mtu muhimu, mpiganaji mahiri katika mambo ya michezo ambaye daima Taswa tutaendelea kumkumbuka.
Tunaipa pole familia yake, Taswa Zanzibar na wanamichezo wengine weote kutokana na msiba huo mkubwa na tupo nao katika kipindi hiki kigumu.
Wakati wa uhai wake Maulid licha ya kuwa kiongozi wa timu mbalimbali ikiwemo kuwa Rais wa timu ya Taifa Jang’ombe iliyopata kushiriki Ligi Kuu Zanzibar, pia amepata kuchezea timu ya Kikwajuni ya Zanzibar.
Pia amepata kuwa msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar(ZFA) kabla ya kujiondoa baada ya uchaguzi wa chama hicho mwaka jana.
Kulingana na taarifa ambazo Taswa imezipata kutoka kwa Katibu wa Taswa Zanzibar, Donisya Thomas ni kuwa taratibu za maziko zilikuwa zikiendelea na kuna uwezekano mkubwa akazikwa leo alasiri. Mungu aiweke mahali pema peponi roho ya Maulid Hamad Maulid.
Amin
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu Taswa
18/10/2011.
DU!POLENI SANA WANA HABARI,KWELI MAULID ALIKUA MPIGANAJI WA KWELI,NAJUA MENGI YATASEMWA SANA JUU YA KIFO CHAKE LAKINI MOLA NDIE ANAEJUA SIRI YA KIFO CHAKE...MBELE YETU NYUMA YAKO KAKA MAULID HAMAD MAULID UMETUACHIA URITHI WA HEKMA,BUSARA NA UCHESHI.MUNGU AIWEKE ROHO YAKO PAHALA PEMA PEPONI.AMEEN
ReplyDelete