TFF YATOA MAAMUZI UTATA WA SMALL KIDS

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliketi Oktoba 16 mwaka huu pamoja na mambo mengine kutolea uamuzi utata uliojitokeza na kukwamisha mechi ya Ligi Daraja la Kwanza kati ya Polisi Iringa na Small Kids ya Mpanda, Rukwa iliyokuwa ichezwe Oktoba 15 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

Utata huo ulisababishwa na uuzwaji wa timu ya Small Kids kwa mmiliki mwingine, huku Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kikipinga kuwa haukuwa halali. Hali hiyo ilisababisha ziwepo timu mbili za Small Kids kwenye mechi hiyo dhidi ya Polisi Iringa.

Baada ya kupitia nyaraka zilizowasilishwa mbele yake zikiwemo za mauzo ya timu hiyo, pamoja na taarifa ya Msimamzi wa Kituo cha Iringa, Eliud Mvella uamuzi wa Kamati ya Mashindano ni kama ifuatavyo;

Small Kids iliyouzwa ndiyo inayostahili kucheza ligi hiyo, kwa vile mwenye mamlaka ya kuuza klabu ni mmiliki mwenyewe na si chama cha mpira wa miguu cha mkoa husika au cha wilaya ambacho klabu ina makao yake. Isipokuwa uhamishaji wa umiliki unapofanyika vyama hivyo vinataakiwa kupewa taarifa.
Vilevile Kamati ya Mashindano imekubali ombi la Small Kids kuhamisha kwa sasa mechi zake kutoka Mpanda baada ya kupokea vitisho kuwa ikienda kucheza huko itakiona cha mtema kuni.
Hivyo Small Kids kwa sasa imeruhusiwa kuchezea mechi zake Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro. Pia mechi kati yake na Polisi Iringa ambayo haikufanyika sasa itachezwa Novemba 1 mwaka huu mjini Iringa.

Katika uamuzi mwingine, Kamati ya Mashindano imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasilisha kesi mbele ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi dhidi ya baadhi ya viongozi wa RUREFA waliosababisha mechi ya Iringa isichezwe na pia kutoa maneno ya vitisho kwa viongozi wa Small Kids.

Post a Comment

Previous Post Next Post