Michuano ya kuwania Kombe la Uhai (Uhai Cup 2011) inayoshirikisha timu za pili (U20) za klabu zote 14 za Ligi Kuu ya Vodacom inatarajia kuanza Novemba 12 mwaka huu katika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boyz) itashiriki michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa ikiwa timu mwalikwa.
Bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba.
Mchezaji bora atapata sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu itapata sh. 300,000. Kila timu inayoshiriki itapatiwa sh. milioni moja kwa ajili ya maandalizi.
Mdhamini pia atagharamia nauli za kuja Dar es Salaam na kurudi kwa timu ambazo zinatoka mikoani. Michuano hiyo itachezeshwa na waamuzi vijana kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Pia mradi wa Campaign Against Malaria nao utasaidia kwa kutoa jezi kwa timu zote zinazoshiriki michuano hiyo.
Kesho (Novemba 5 mwaka huu) saa 4 asubuhi kutakuwa na mkutano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu zenye timu shiriki na baadaye kufanyika upangaji ratiba.