Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenella Mukangara leo (Machi 10 mwaka huu) amechangia sh.
milioni moja kwenye uzinduzi wa akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa
kuichangia timu hiyo ambayo inashiriki michuano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake
(AWC).
Akizungumza kwenye hafla hiyo
iliyofanyika Dar es Salaam, Dk. Mukangara alisema ni jukumu la kila Mtanzania
kuichangia Twiga badala ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuachiwa
pekee mzigo huo wa kuendesha timu hiyo.
Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa
kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa
kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Kwa Waziri Dk. Mukangara
kuchangia sh. milioni moja alifanya mihamala miwili.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais
wa TFF, Athuman Nyamlani alisema Twiga Stars kwa sasa haina mdhamini na
Shirikisho limekuwa likibeba mzigo wa kuhakikisha inashiriki katika mechi za
kirafiki na mashindano mbalimbali kwa vile imekuwa ikifanya vizuri.
Twiga Stars inayofundishwa na
kocha Charles Boniface Mkwasa iko kwenye raundi ya pili ya mashindano ya Kombe
la Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini
Addis Ababa.
Katika raundi ya kwanza,
Twiga Stars iliitoa Namibia kwa jumla ya mabao 7-2. Ilishinda ugenini 2-0 na
kuibuka na ushindi mnono nyumbani wa mabao 5-2. Fainali za AWC zitafanyika
Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)