HOMA ya pambano la soka la wasanii wa vichekesho vya luninga
‘komedi’ wa kutoka mkoani Dar es Salaam na jijini Mwanza ‘Rock City’, imepanda
baada ya mastaa hao kutambiana kuwa kesho Jumamosi katika Uwanja wa CCM Kirumba
patachimbika.
Tayari wachekeshaji wa Dar es Salaam
wamewasili Mwanza kwa mchezo huo maalumu wenye lengo la kutoa burudani,
kumaliza ubishi wa nani zaidi kati yao
na kujenga ushirikiano kwa wasanii hao.
Mechi hiyo imekuwa gumzo kubwa katika jiji la Mwanza na
mikoa ya jirani ya Kanda ya Ziwa, baada ya wachekeshaji Kingwendu na Bambo
kuwasili mkoani humo na kutamba kupitia vyombo vya habari kwamba, wamekwenda
kutafuta ushindi katika mchezo huo.
Kwa mujibu wa mratibu wa mechi hiyo iliyoandaliwa na Kampuni
ya Brayance Promortes, Pearson Samwel, maandalizi yote yamekamilika na
kinachosubiriwa siku ya mchezo ili kumaliza ubishi uliotawala wa komedi wa Dar es Salaam na Mwanza
kina nani wanaweza kusakata soka.
“Tunashukuru tumekamilisha maandalizi yote na wasanii wote
wamefanya mazoezi kwa ajili ya kucheza soka kwa dakika 90 na wanatazamia kutoa
ushindani mkubwa kati yao ,”
alisema Samwel kutoka Mwanza.
Alisema kuwa viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh 2,000
mzunguko na sh. 5,000 katika jukwaa kuu na mpaka jana walikuwa wanakamilisha
taratibu za mwisho kupata mgeni rasmi.
Wasanii kutoka Dar es Salaam watakaoshuka ndani ya CCM
Kirumba siku hiyo ni Kingwendu, Sharo Milionea, Mboto, Senga, Pembe, Bambo,
Mtanga, Mau, Ringo na Chilly, Defender, Zimwi, Muhogo Mchungu, Masele, Erick,
Kiuno na Hawa.
Timu ya wachekeshaji wa Mkoa wa Mwanza inaundwa na Babu
Mkombe,Sharobaro wa Kihaya, Mchele, Chugu, Ngosha, Brother K, Mama Brandina,
Msimbe wa ukweli,Okech Okech, Kafuku Kaukananga, Mzee Dude, Itagata,
Malapulapu, Choko na Tengambili.
Wasanii wengine watakuwepo siku hiyo ni Tatu Mkate wa
Arusha, Avodia Tolu, Mrefu kwenda chini na Jully Tax, ambao wamepania kuwafunga
wachekeshaji wenzao wa Dar es Salaam .