MSHAMBULIAJI wa timu
ya soka ya Azam Fc na kinara wa mabao kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara, John
Raphael Bocco ‘Adeboyor’ ametangaza
kustaafu kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Bocco ambaye ambaye amekuwa mmoja ya wachezaji chaguo la kocha
mkuu wa Stars Jan Poulsen,amefikia hatua hiyo kutokana na kuchoshwa na kuzomewa
na mashabiki wa soka kila anapopangwa katika kikosi cha Stars na baada ya hatua
hiyo sasa atabaki kuelekeza nguvu zake katika timu yake ya Azam.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za leo, nyota
huyo ameshawasilisha barua kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) juu ya uamuzi
wake huo na kuiomba TFF kulikemea suala la wachezaji kuzomewa wakiwa na jezi za
Taifa kama walivyokemea uharibifu wa
mali za Uwanja wa Taifa.
Mkurugenzi wa Mashindano wa
TFF Saad Kawemba alisema bado
hawajapokea rasmi barua ya BOcco huku akishangazwa na hatua hiyo na kusema kama ni kweli mchezaji huyo
anahitaji ushauri nasaha.
Alisema tatizo linaloonekana ni umri mdogo alionao mchezaji
huo ndio unamfanya ajisikie vibaya mashabiki kumzomea hivyo kikubwa
kinachohitajika ni viongozi wa TFF pamoja na timu yake ya Azam Fc kukaa naye na
kumpa ushauri.
“Hahaha amejiuzulu kuichezea Stars kwa kipi?mimi nadhani
umri ndio unamsumbua sasa kwa udogo alionao anastaafu kuichezea Stars hiyo
inaleta maana kweli, kimsingi anahitaji ushauri toka wakubwa zake kwani huwezi
kuacha kucheza kwa sababu ya kuzomewa na mashabiki kwa umri huo akistaafu Stars
ndio inakuwaje?”Alihoji
“Kuzomea ni jambo la kawaida kwa wachezaji, amezomewa Et’oo
(Samwel) na kuitwa nyani au wachezaji
wangapi wakubwa duniani wanazomewa na kudhalilishwa kabisa lakini wanapuuza na
kuendelea na kinachowahusu,”Aliongeza Kawemba.
Aidha, Kawemba alisema pindi watakapoipata rasmi barua hiyo
watakaa na mchezaji huyo na kuongea naye, huku pia wakiangalia ni jinsi gani
watatoa elimu kwa mashabiki kuachana na tabia za zomea zomea ambazo zinawavunja
moyo wachezaji.