Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana
Machi 24 mwaka huu imepitisha michuano ya Ligi ya Taifa Ngazi ya Taifa
inayoshirikisha mabingwa wa mikoa ianze Aprili 22 mwaka huu kwenye vituo vitatu
tofauti.
Wakati Machi 26 mwaka huu
ndiyo ilikuwa mwisho kwa vyama vya mikoa kuwasilisha TFF majina ya mabingwa wao,
ni mikoa minne tu iliyomudu kufanya hivyo kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya
TFF.
Mikoa hiyo na mabingwa wake
kwenye mabano ni Kigoma (Kanembwa FC ya Kibondo), Ruvuma (Mighty Elephant ya
Songea), Kilimanjaro (Forest FC ya Siha) na Dodoma (CDA ya Dodoma
Mjini).
Hivyo Kamati ya Mashindano imeongeza muda
hadi Aprili 9 mwaka huu kwa mikoa ambayo haijawasilisha majina ya mabingwa wao
iwe imefanya hivyo. Kwa itakayoshindwa ndani ya muda hiyo, mabingwa wao
hawatapata fursa ya kucheza ligi hiyo.
Kamati imetoa pongezi kwa
mikoa hiyo minne kwa kuhakikisha imechezesha ligi yao kwa mujibu wa kalenda ya
matukio ya TFF. Pia imepanga makundi matatu ya ligi hiyo. Kundi A lina mikoa ya
Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Lindi na Mtwara.
Kundi B lina mabingwa wa
mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Singida na Dodoma.
Kundi C ni Dar 1, Dar 2, Dar 3, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na
Manyara.
TFF inakaribisha maombi ya
uenyeji kwa kila kundi. Taarifa rasmi itatumwa kwa vyama mikoa kueleza masharti
ya kutimiza kabla ya mkoa kupewa kituo cha ligi hiyo.
Mshindi katika kila kundi na
washindwa bora (best losers) wawili kutoka kwenye makundi yenye timu nane
watapanda daraja msimu ujao kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Pia timu zinatakiwa ziwe
zimefanya usajili wa wachezaji kufikia Aprili 10 mwaka huu wakati Aprili 11-18
itakuwa ni kipindi cha kutangaza majina na pingamizi.