Na Mwandishi Wetu
SERIKALI
imeipongeza Kampuni ya Heineken Afrika Mashariki kwa kuiteua Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi zinazotembelewa na Kombe la UEFA, huku ikiiomba kuwekeza
kwenye sekta ya michezo hapa nchini hususan, timu ya taifa ya wanawake, Twiga
Stars.
Pongezi na
maombi hayo yalitolewa juzi usiku na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, katika hafla ya kulishuhudia kombe hilo iliyofanyika kwenye
Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski jijini Dar es Salaam.
Dk. Mukangara
alisema wanatambua uwepo wa Heineken hapa nchini, kwani wanaziona bidhaa zao,
hivyo kwa namna moja ama nyingine wanachangia uchumi wa nchi kupitia kodi.
Alisema kwa
uamuzi huo wa kulileta kombe hilo maarufu
duniani, wameongeza chachu na hamasa ya michezo hapa nchini, lakini litakuwa
jambo bora kama watawekeza kwenye michezo hapa
nchini na kuisaidia Twiga Stars, hasa ukizingatia inajituma na kuonyesha
kiwango bora.
Katika hafla
hiyo, ambayo waalikwa walipata nafasi ya kupiga picha na kombe hilo,
ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utawala Bora, Mathias Chikawe, Mbunge wa Bariadi Magharibi, John Cheyo,
Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni,
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake, Lina Madina
Mhando na wengineo.