Na Dina Ismail
KLABU ya soka ya Simba imesema haina
haja ya kwenda kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa
raundi ya kwanza ya kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya
Algeria, imefahamika.
Simba imevuka hatua hiyo baada ya
kuisukumiza nje ya michuano hiyo Kiyovu Sport ya
Rwanda hivyo itakwaana na Wa Algeria
hao mwishoni mwa wiki ijayo.
Akizungumza kwa simu jana Mwenyekiti
wa Simba, Alhaj Ismail Rage alisema kwamba wameona hakuna haja ya kwenda kujinoa
nje ya nchi kutokana na hali ya hewa ya Algeria kuwa
sawa na ya hapa nchini.
Alisema pamoja na hali ya hewa
wamebaini kuwa wapinzani wao si timu ya kutisha sana
hivyo wameona waendelea kujinoa hapa nchini kupitia michezo ya ligi kuu soka
Tanzania Bara inayoendelea kwa sasa.
“Maandalizi ya Algeria
yanakwenda vema ingawa hayatupi presha kubwa sana
kwa kuwa tumeshazipata taarifa zao kwa kiasi kikubwa na mwalimu anazifanyia
kazi...lakini suala la kambi litaendelea kuwa hapa nchini na huko tutaenda siku
chache kabla ya mchezo,”Alisema Rage.
Katika hatua nyingine, kikosi cha
Simba kinatarajiwa kuondoka mjini Dodoma leo kwenda Morogoro tayari kwa mchezo
wake wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa keshokutwa
katika katika dimba la Jamhuri.