Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari Utamaduni na Michezo, Dkt. Emmanuel Nchimbi
atakuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa Mtandao wa Wasanii Tanzania
(SHIWATA) ambao utafanyika ukumbi wa StarLight, Dar es Salaam Jumamosi (kesho)
Machi 31, 2012 kuanzia saa 4 asubuhi.
Katika mkutano huo
wanachama watapata taarifa kuhusu mikakati ya awamu wa pili ya ujenzi wa nyumba
178 kati ya 1,000 zinatarajiwa kujengwa katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Caasim Taalib alisema ,paka sasa
imejenga nyumba tano(5)za awali kwa gharama ya sh. 33,789,097 ambapo mbili kati
ya hizo tayari zimekabidhiwa kwa wanachama Josephine Moshi na Flora Kafwembe.
Alisema nyumba hizo ambazo zimejengwa kwa tofali za
kupachika na nyingine kwa tofali za saruji zimeezekwa kwa vigae vya kisasa
kutoka Wakala wa Taifa wa Utafiti na Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu (NHBRA)
ambazo zimekuwa kivutio kikubwa katika kijiji cha Mwanzega, wilayani Mkuranga
kiasi cha kufafanishwa na kijiji cha Hollywood ya Marekani na kukibatiza kijiji
hicho kuwa cha Tanzawood.
Mwenyekiti Taalib alisema mpaka sasa makampuni mbalimbali za
nchini pamoja na wafadhili kutoka Saudi Arabia ni baadhi ya wafadhili
walionesha nia ya kuchangia ujenzi wa kijiji hicho.
Alisema mpaka sasa viongozi mbalimbali wamefika kuona ujenzi
wa nyumba hizo ambazo zimepewa baraka na Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo
na Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Henry Clemence.