1.Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika tarehe 25
Machi 2012 ilijadili mkanganyiko na mgogoro uliopo wilayani Babati kuhusu
uchaguzi wa viongozi wa chama cha mpira wa Miguu Wilaya ya Babati (BDFA).
2. Kamati ilibaini kuwa mgogoro uliojitokeza
kuhusu uchaguzi wa BDFA umesababishwa na Kamati ya Uchaguzi ya Mkoa wa Manyara
kwa kutotimiza wajibu wake wa kusimamia uchaguzi wa BDFA na mgogoro wa uongozi
ndani ya BDFA uliosababisha kuundwa kwa Kamati mbili za uchaguzi kinyume na
matakwa ya Katiba ya BDFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imebaini na kujiridhisha pia kuwa, mgogoro kuhusu uchaguzi wa
viongozi wa BDFA umepanuka zaidi kutokana na uongozi wa BDFA kutotekeleza
maagizo ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF yaliyotolewa kwa BDFA na pia Kamati ya Uchaguzi ya MRFA kukaidi maagizo ya
Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyoitaka Kamati ya Uchaguzi ya MRFA kusimamisha
chaguzi zote Mkoani Manyara ili kuyapatia ufumbuzi mataizo ya uchaguzi
yaliyojitokeza Mkoani Manyara.
3.Kwa kuwa Kamati ya Uchaguzi ya MRFA imekaidi kutekeleza maagizo ya TFF
kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF na Katiba ya MRFA na pia kwa
kutotimiza kwa makusudi wajibu wake wa
kusimamia kwa weledi chaguzi za
wanachama wa MRFA na kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Kamati
ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake yaliyoainishwa katika Katiba ya TFF Ibara
ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya ya 6, Kanuni za Uchaguzi za wanachama
wa TFF Ibara ya 10(6), 26(2) na 26(3) imeamua yafuatayo:
(i) Imefuta na
kutengua matokeo ya chaguzi za viongozi wa BDFA zilizofanyika tarehe 19
Februari 2012 na tarehe 11 Machi 2012.
(ii) Imezifuta
Kamati za Uchaguzi za BDFA.
(iii) Imeifuta
Kamati ya Uchaguzi ya MRFA.
4.Kutokana na maamuzi hayo, TFF inaiagiza Kamati ya Utendaji ya MRFA
kuchagua Kamati mpya ya Uchaguzi ya MRFA itakayozingatia matakwa ya Katiba ya
TFF na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF katika kutekeleza majukumu
yake. Uongozi wa MRFA unatakiwa
kuhakikisha kuwa Kamati ya Utendaji ya
BDFA inateua Kamati mpya ya uchaguzi kwa
mujibu wa Katiba ya BDFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF katika
Kipindi cha mwezi mmoja kuanzia tarehe ya barua hii, ili kuanza mchakato wa
uchaguzi wa viongozi wa BDFA chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya MRFA.
Hamidu Mbwezeleni
MAKAMU MWENYEKITI
KAMATI YA UCHAGUZI –TFF